Wamarekani nchini DRC wakabiliwa na hukumu ya kifo baada ya jaribio la mapinduzi

Wamarekani nchini DRC wakabiliwa na hukumu ya kifo baada ya jaribio la mapinduzi

Raia wa Marekani Marcel Malanga na Taylor Christian Thomson walipewa hukumu yao mahakamani nchini DRC
Marcel Malanga (katikati, safu ya pili) anakaa miongoni mwa watuhumiwa wengine wa jaribio la mapinduzi lililofeli katika Gereza la Ndolo huko Kinshasa / Picha: AFP

Takriban watu 50, wakiwemo raia watatu wa Marekani na Mbelgiji mmoja, walishtakiwa Ijumaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kile jeshi lilichoita jaribio la mapinduzi.

Matendo ya Wamarekani watatu yalikuwa "yanaadhibiwa kwa kifo", hakimu Freddy Ehume aliambia mahakama ya kijeshi katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa.

Marcel Malanga na Taylor Christian Thomson, wote wenye umri wa miaka 21, na Benjamin Reuben Zalman-Polun mwenye umri wa miaka 36 walikuwa wa kwanza kusimama mbele ya hakimu kusikia mashtaka yanayosomwa dhidi yao.

"Matendo haya yanaadhibiwa kwa kifo," alisema hakimu mkuu wa mahakama ya kijeshi ya Kinshasa-Gombe kwa watatu hao.

Wanadiplomasia walikuwepo

Wengine wapatao 50 walifuata mmoja baada ya mwingine chini ya hema kubwa kwenye viwanja vya gereza la kijeshi la Ndolo kusikia mashtaka.

Wote walionekana wakiwa wamevaa sare za gereza za buluu na njano katika kesi yao, ambayo ilianza saa 5:40 asubuhi (1040 GMT) na ilifuatiliwa na wanadiplomasia wa magharibi, waandishi wa habari na wanasheria.

Jaribio la mapinduzi linalodaiwa lilitokea Mei 19 wakati wanaume wenye silaha waliposhambulia nyumba ya Waziri wa Uchumi Vital Kamerhe mapema asubuhi kabla ya kuelekea kwenye Palais de la Nation iliyo karibu ambayo inahifadhi ofisi za Rais Felix Tshisekedi.

Walionekana wakipigwa picha wakionesha bendera ya Zaire - jina la nchi ya Afrika ya Kati wakati wa utawala wa dikteta wa zamani Mobutu Sese Seko - na wakitamka kwa sauti kubwa kwamba serikali ya Rais wa sasa Felix Tshisekedi imekwisha.

Jeshi baadaye lilitangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba vikosi vya usalama vilizuia "jaribio la mapinduzi ya serikali".

Lengo halieleweki

Njama hiyo iliyodaiwa iliongozwa na Christian Malanga, mwanaume wa Kongo ambaye alikuwa "amepata uraia wa Marekani" na ambaye aliuawa na vikosi vya usalama, msemaji wa jeshi Jenerali Sylvain Ekenge amesema.

Mwanae, ambaye ni raia wa Marekani, alikuwa mmoja wa Wamarekani watatu waliofikishwa kizimbani Ijumaa.

Ekenge alisema wapatao 40 wa washambuliaji, wa "taifa mbalimbali", walikamatwa na wengine wanne kuuawa, akiwemo Malanga.

Lengo la tukio hilo linalodaiwa bado halieleweki lakini serikali ililaani kuwa ni jaribio la "kuvuruga" "taasisi" za nchi hiyo kubwa.

Mtaalam wa kijeshi

Wanawake wanne ni miongoni mwa washtakiwa, pamoja na Mbelgiji mmoja, Jean-Jacques Wondo.

Wondo, mtaalamu wa kijeshi mwenye asili ya Kongo, alikamatwa siku mbili baada ya tukio hilo, Mei 21.

Anashtakiwa kwa kuwa "mshirika mwenza wa Christian Malanga" kwa "kutoa usafiri" kwa wanasiasa wa njama hiyo, wakili wake alisema.

Wondo alikanusha mashtaka dhidi yake na atajitetea, wakili Masingo Shela aliongeza.

Kulingana na hati ya mahakama, jumla ya washtakiwa 53 wanashitakiwa, pamoja na Christian Malanga, ingawa amekufa.

Mashtaka ni pamoja na "shambulio, ugaidi, umiliki haramu wa silaha na risasi za kivita, jaribio la mauaji, ushirikiano wa kihalifu, mauaji (na) ufadhili wa ugaidi", kulingana na hati hiyo.

AFP