Malawi inawahifadhi zaidi ya wakimbizi 70000 wengi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi/ Picha: Reuters

Maafisa nchini Malawi wamesema kuwa wamewakamata zaidi ya wakimbizi 400 na watu wanaotafuta hifadhi katika mji mkuu Lilongwe.

Serikali ilisema Alhamisi kuwa, waliokamatwa walikataa kurejea katika kambi ya wakimbizi nje kidogo ya mji mkuu.

Wizara ya Usalama wa Ndani imesema kuwa watu 408, wakiwemo watoto zaidi ya 100 wanazuiliwa, kufuatia msako wa siku mbili uliofanywa katika vitongoji mbali mbali mjini Lilongwe.

Operesheni hiyo imefanywa miezi miwili baada ya serikali kuweka sharti kwa wakimbizi kurejea kambi ya Dzaleka, iliyoko kilomita 40 kaskazini mwa mji mkuu.

"Muda tuliowapa umemaizika," msemaji wa wizara Patrick Botha aliambia shirika la AFP.

"Tumewaonya kuwa wakikosa kutii amri tutatumia polisi kuwahamisha kwa lazima." Aliongeza Botha.

Wakimbizi wengi na wanaotafuta hifadhi nchini Malawi wametokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayokabiliwa na mapigano, na wengine wengi wanatokea Burundi.

Waliokamatwa wanafanyiwa uchunguzi katika gereza moja kujua iwapo baadhi yao wamo nchini humo kinyume cha sheria.

Maafisa pia wamewashutumu baadhi ya wakimbizi hao kuendesha biashara bila vibali.

Kiongozi wa jamii ya Warundi mjini Lilongwe Bantubino Leopold, amesema kuwa ameshangazwa na msako huo wa polisi kwani waliahidiwa kupewa ulinzi.

"Tuna makubaliano yanayowaruhusu wakimbizi wanaoweza kujisimamia kibiashara waendelee na kazi zao ili waisitegemee misaada." Leopold aliambia AFP.

Malawi inawahifadhi zaidi ya wakimbizi 70,000 kwa mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR.

TRT Afrika