Na Kudra Maliro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Katika kambi ya wakimbizi ya Kanyaruchina huko Kivu Kaskazini, DRC, kikundi cha wacheza densi hupata hadhira ya watu huku wakicheza ngoma na sarakasi za kuvutia zinazoibua shangwe na nderemo kutoka kwa watazamaji waliokusanyika.
Wacheza densi wanatumbuiza kama sehemu ya shughuli za kusherehekea Siku ya Densi Duniani 2024, iliyoandaliwa na Collectif des Danseurs du Kivu, kusaidia watu waliokimbia makazi yao nchini DRC kukimbia kiwewe cha vita.
Siku ya Densi Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 29 Aprili na ni fursa nyingine ya kukumbusha dunia juu ya tiba ya kucheza, ambayo inaweza kuponya makovu mengi ya kihisia.
Kasereka Kasolene, anayejulikana kama Taylor Cruzz, dansa mtaalamu mwenye umri wa miaka 23 na mwanachama wa Collectif des Danseurs du Kivu, alihudhuria hafla hiyo huko Kanyaruchina, kilomita 20 kutoka Goma.
"Tuko kumi kati yetu, tulijaribu kuwafundisha ngoma za asili, hip-hop, breakdance, ngoma ya kisasa na salsa," Kasolene anaiambia TRT Afrika.
Mapigano ambayo yamepamba moto kwa miaka mingi kati ya waasi na wanajeshi wa serikali yamewafanya mamilioni ya watu kuyahama makazi yao mashariki mwa DRC.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 7.2 wamekimbia ghasia zinazofanywa na makundi yenye silaha mashariki mwa DRC.
Maelfu wamekuwa wakiishi katika mazingira hatarishi katika kambi ya Kanyaruchinya, kilomita 20 kutoka Goma.
Waandalizi wanasema zaidi ya watu 1,500 waliokimbia makazi yao walihudhuria sherehe hiyo, huku wengi zaidi wakitarajiwa kuhudhuria katika siku zijazo.
"Kila mara mtu ana densi inaonekana kuponya majeraha yasiyoonekana. Tabasamu ziligeuka kuwa vicheko, na miili iliyochoshwa na maisha magumu ya kila siku kambini ilizidi kupata nguvu," Kasolene alisema.