Bei ya mafuta nchini kneya imeongezeka nchini Kenya / Picha: AP

Bei ya mafuta nchini Kenya imefikia kiwango cha juu zaidi kihistoria na kuvuka alama ya shilingi 200 ya Kenya ambayo ni takriban $1.36.

Mdhibiti wa nishati nchini, EPRA, alitangaza bei mpya Alhamisi jioni katika ukaguzi wake wa kila mwezi.

Bei hizo mpya zitasalia kati ya Septemba 15 na Oktoba 14, wakati marekebisho mengine ya bei yatakapofanywa.

"Bei ya mafuta ikiongezeka inamaanisha kuwa gharama yetu ya maisha itaongezeka," Paul Njoroge mkazi wa jiji la Nairobi anasema.

"Kwa nini serikali haioni kuwa tayari tumefinyika, hii inamaanisha bei ya usafiri itaongezeka na hapo bei ya bidhaa zingine," Rose Musitwa, mkazi mwingine wa Nairobi asema.

Katika mji wa pwani wa Mombasa, ambao una bandari kuu inayopokea mafuta ghafi kutoka nje, lita moja ya petroli itagharimu dola 1.42, huku dizeli ikiuzwa kwa dola 1.35.

Bei hizo mpya za juu zitasalia kati ya Septemba 15 na Oktoba 14 mwaka huu / Picha: Reuters 

Robert Ruto ni dereva teksi, anasema serikali ikiongeza bei ya mafuta basi naye itamlazimu kuongeza bei kwa wateja.

"Nina mteja ambaye hunilipa takriban dola 12 kila siku kumpeleka mtoto wake shuleni na kumrudisha nyumbani, Sasa hata sijui nimwambie vipi kwamba atahitaji kuongeza ada hii kidogo, hata naona aibu kwani tayari naona analipa hela nyingi," Ruto anasema.

Mafuta ya taa, kwa upande mwingine, yatauzwa kwa dola 1.36.

Lita moja ya petroli Nairobi sasa itauzwa kwa dola 1.44, huku dizeli ikigharimu dola 1.37 na mafuta ya taa dola 1.38.

Kuondolewa kwa ruzuku

Rais wa Kenya William Ruto, ambaye alitimiza mwaka mmoja madarakani juzi Jumatano, aliondoa ruzuku ya mafuta baada ya kuchukua mamlaka mnamo Septemba 2022.

Rais wa Kenya William Ruto aliondoa ruzuku ya mafuta akidai inagharimu nchi pesa mingi/ picha : Others 

Mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, alianzisha mpango wa ruzuku mnamo Oktoba 2021 ili kuwaepusha Wakenya dhidi ya gharama ya juu ya maisha.

Huku akihalalisha uamuzi wake wa kuondoa mpango wa kutoa misaada, Ruto alisema kuwa Kenya inadaiwa madeni makubwa kuendeleza mpango huo, ambao "ulikuwa unawanufaisha watu wachache, ilhali Wakenya bado wanapitia gharama kubwa ya maisha."

Mnamo Agosti 2023, katika jitihada za kuzuia bei ya mafuta kuvuka alama ya Ksh200 (alama ya $1.36), Ruto alirejesha kwa muda ruzuku ya mafuta, hatua ambayo vyombo vya habari vya Kenya viliiita "U-turn" kwenye msimamo thabiti wa rais kuhusu ruzuku.

Mapitio ya hivi punde yanaonyesha kwa mara ya kwanza bei ya mafuta nchini Kenya imepanda zaidi ya alama ya Ksh200 ($1.36).

TRT Afrika