Boti ya wahamiaji iliyokuwa ikijaribu kuvuka bahari ya Mediterania imepinduka na kusababisha vifo vya watu wanane akiwemo mtoto mdogo.
Maofisa ulinzi wa pwani ya Italia walifanikiwa kuokoa watu 23, kulingana na shirika la habari la ANSA la Italia.
Chombo hicho kinaripotiwa kuzama katika kisiwa cha Lampedusa, lililo kilomita 55.
Katika taarifa za awali za manusura wa ajali hiyo, ilielezwa kuwa kuna watu wengine walipotea baharini wakati boti hiyo ilipozama, lakini idadi yao haijajulikana.
Kati ya waathirika wa tukio hilo, wapo walipoteza uhai kwa sasabu ya kupoteza joto la mwili.
Filippo Mannino, meya wa kisiwa cha Lampedusa, amesema kuwa eneo hilo limeshtushwa na vifo vya watu hao
"Hivi sasa, miili nane, ikiwa ni pamoja na ya msichana mdogo, imeletwa. Hii imekuwa hesabu isiyo na mwisho. Hali ya bahari ni mbaya na wafanyabiashara wa binadamu wanaendelea kuwapeleka watu hawa maskini, waliokata tamaa kwenye boti ndogo ambazo haziwezi hata kuelea. Hadithi ni ile ile kila siku.
Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa linasema kuwa wahamiaji 385 wamepoteza uhai wao katika bahari ya Mediterranean toka kuanza kwa mwaka hadi kufikia Aprili 8.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia, idadi ya wahamiaji waliowasili nchini kwa njia ya bahari kuanzia Januari 1 hadi Aprili 10 mwaka huu ilifikia 15,774 ikilinganishwa na 31,128 katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Msafara wa uhamiaji na ajali zinazofuata za boti zinaendelea katika eneo la kati la Mediterania, mojawapo ya njia za uhamiaji zisizo za kawaida zinazotumiwa kutoka Afrika hadi Ulaya.