Rais wa Zambia Haikainde Hichilema Photo: AA / Photo: AP

Mamlaka ya Zambia imetuma wanajeshi kuharakisha juhudi za uokoaji kwa takriban waumini wanane waliotoweka kufuatia ajali ya boti.

Boti iliyobeba waumini 44 wa Kanisa la Waadventista Wasabato ilipinduka siku ya Ijumaa kwenye Ziwa Bangweulu katika Mkoa wa Luapula. Watu 28 waliokolewa, huku 11 wakiripotiwa kufariki.

Mkuu wa polisi Gloria Mulele alisema waathiriwa walikuwa wakisafiri kwa meli kuelekea kwenye mpango wa kanisa. "Walionusurika wamekimbizwa katika hospitali ya wilaya kwa matibabu," Mulele alisema. Katika taarifa yake, alisema watu waliopotea ni kati ya umri wa miaka miwili na 28.

''Nikiwa ziwani, mawimbi makali na upepo ambao ulikumba ziwa hilo uligonga boti na kupinduka huku nahodha akishindwa kuidhibiti," aliongeza.

Lakini kanisa lilisema taarifa rasmi zilizopokelewa zilionyesha kuwa watu 29, ikiwa ni pamoja na nahodha, waliokolewa, wakati 15 walikuwa bado hawajaonekana.

"Hadi sasa, wanne kati ya waliookolewa, wamelazwa hospitalini, na wengine wameruhusiwa kwenda nyumbani," kanisa lilisema.

Msemaji wa Serikali Chushi Kasanda alisema katika taarifa yake kuwa maiti nane zimeopolewa na nane bado hazijapatikana.

"Ni kwa mshtuko mkubwa na huzuni kwamba Rais amesikia juu ya ajali ya boti iliyoripotiwa kuwabeba waumini 44 wa kwaya ya kanisa la Waadventista Wasabato, ambayo ilipinduka kwenye Ziwa Bangweulu.

Uchungu wa kupoteza maisha ya vijana wengi katika mkasa mmoja wa ukubwa huu hauwezi kuvumilika,” Kasanda alisema katika taarifa yake kwa njia ya barua pepe.

Alisema vikosi vya baharini vimetumwa kusaidia shughuli za utafutaji na uokoaji akiongeza kuwa Rais Hakainde Hichilema ameagiza mashirika ya serikali kutoa majeneza, chakula na msaada mwingine kwa nyumba za mazishi ili kupunguza mzigo kwa kanisa na familia zilizofiwa.

TRT Afrika na mashirika ya habari