Rais Ramaphosa alisema hayo alipomkaribisha Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong. Picha/Reuters

Viongozi wa nchi sita za Kiafrika watasafiri hadi Ukraine na Urusi "hivi karibuni" ili kujaribu kupatanisha nchi zinazozozana, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema Jumanne.

Hakufichua tarehe ya kuondoka kwao wala taarifa za kina kuhusu safari ya viongozi hao wa Zambia, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Misri na Afrika Kusini, kama ilivyoripotiwa na shirika la habari la Reuters.

Alisema hayo alipomkaribisha Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong.

Cyril Ramaphosa alisema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky wamekaribisha hatua hiyo ya viongozi wa Afrika, na "kukubali kuwakaribisha huko Moscow na Kyiv."

Ramaphosa alisema alizungumza "kwa simu" na Rais Putin na Zelensky wikendi iliyopita.

"Sababu yetu kubwa ya kutaka kwenda nchini humo ni kujadili juhudi za kutafuta amani ili kumaliza mgogoro wa kutisha wa Ukraine unaosababisha vifo vya watu na kuathiri nchi za Afrika," alisema.

Rais Ramaphosa alisema kuwa wamemjulisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Umoja wa Afrika kuhusu mpango huu na wote walipokea mpango huo.

TRT Afrika na mashirika ya habari