Viongozi kutoka bara la Afrika ni miongoni mwa viongozi wa mataifa mbalimbali waliowasili Beijing China ili kushiriki mkutano wa kimataifa wa ukanda na barabara nchini humo.
Rais wa Kenya William Ruto, Waziri mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia, Rais Denis Sassou Nguesso wa Congo, naibu Rais wa Nigeria Kashim Shettima ni miongoni wa Waafrika waliowasili Beijing miongoni mwa wakuu wa nchi na serikali tofauti.
Mkutano huo wa ukanda na barabara kwa ushirikiano wa kimataifa, utaanza rasmi Jumanne huku serikali ya China ikiwa mwenyeji wao na kuwapokea wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 130 na mashirika 30 ya kimataifa waliofika kushiriki mkutano huo, Beijing.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa China Hua Chunying ametangaza kuwa mkutano huo wa tatu wa Ukanda na Barabara kwa Ushirikiano wa kimataifa utafanyika Beijing kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 18 Oktoba.
Rais wa china Xi Jinping anatarajiwa kuhutubia mkutano huo ambao unafanyika chini ya kauli mbio " Ushirikiano wa Ukanda wa hali ya juu na barabara: pamoja kwa maendeleo ya kawaida na ustawi.”
Mkutano huu ni wa kwanza kufanyika uso kwa uso tangu 2019 kufuatia uviko-19 na unatarajiwa kushuhudia ushiriki wa marais, makamu wa rais, na mawaziri wakuu.
Rais wa urusi Vladimir Putin ni mmoja wa viongozi wengine mashuhuri wakiwemo pia na Rais wa Indonesia Joko Widodo, Rais wa serbia Aleksandar Vucic, Waziri mkuu wa Misri Mostafa Madbouly, na Waziri mkuu wa Pakistan Anwaar Ul Haq Kakar.