China, Tanzania na Zambia zimekubaliana kuboresha reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) yenye urefu wa kilomita 1860.
Utiaji saini wa makubaliano hayo, umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika na China (FOCAC), unaoendelea mjini Beijing, ukishuhudiwa na Rais Xi Jinping wa China, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Hakainde Hichilema wa Zambia.
Reli ya TAZARA, inayounganisha nchi za Tanzania na Zambia, ilijengwa kati ya mwaka 1970 na 1975, kupitia mkopo usio na riba kutoka China, na ilianza rasmi kufanya kazi mwezi Julai mwaka 1976.
"China ina nia ya kutumia mkutano huu katika kuifufua reli kati ya Tanzania na Zambia, na vile vile kuimarisha mtandao wa njia ya reli na bahari, akisisitiza kuwa ni ishara ya uimarishaji wa mradi mkubwa wa miundombinu ya barabara na Reli," alisema Rais Xi.
Mapema mwaka huu, Benki ya Dunia iliidhinisha Dola Milioni 270 ili kurahisisha usafiri wa treni kati ya Tanzania na Zambia na kukuza biashara kusini mwa Afrika.
Kabla ya ujio wa China, Tanzania na Zambia zilikuwa na lengo la kujenga mradi wa TAZARA. Hata hivyo, mradi huo ulishindwa kutekelezwa kutokana na kuwa ungegharimu fedha nyingi.
Hata baadhi ya nchi za Magharibi zilikataa kufadhili mradi huo, zikisisitiza kuwa "haukuwa na tija kiuchumi.”
Septemba 5, 1967, makubaliano ya ujenzi wa reli ya TAZARA ulikamilika mjini Beijing kati ya serikali za China, Tanzania na Zambia.
Mpango wa awali ulikuwa ni kujenga reli itakayoanzia eneo la Kidatu kwa upande wa Tanzania hadi Kampoyo nchini Zambia.
Jumla ya wafanyakazi 38,000 kutoka Zambia na Tanzania walishiriki katika ujenzi huo wa kihistoria, huku 13,500 wakiwa ni kutoka China.
Zaidi ya wafanyakazi 160, 64 wakiwa ni wachina walipoteza maisha wakati wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1860.