Na Sylvia Chebet
Kukosekana kwa usawa kidogo katika ugavi wa chakula kunaweza kusababisha mgogoro.
Wakati Namibia inapambana na uhaba mkubwa wa chakula unaosababishwa na ukame mkubwa ambao umeangamiza mazao katika nchi nyingi za Kusini mwa Afrika, maadili ya usambazaji wa chakula yametiliwa shaka.
Huku karibu nusu ya wakazi wake milioni 3.03 wakiwa wamebaki na chakula kidogo, serikali imelazimika kuchukua uamuzi mgumu - kuchinja wanyamapori kulisha familia zenye njaa.
"Kama hatutachukua hatua, tutakuwa na vifo vingi kutokana na hali ya ukame ambayo tunakabiliana nayo," Romeo Muyunda, msemaji wa wizara ya mazingira ya Namibia, anaiambia TRT Afrika.
"Kutakuwa na upungufu wa malisho ya mimea na maji ya kunywa kwa wanyama na watu. Hii itasababisha migogoro zaidi kati ya watu na wanyama. Na kunapokuwa na migogoro ya aina hiyo, wanyama daima watakuwa katika hali mbaya."
Uchinjahi huo umeanza, na kwa familia nyingi zenye njaa, kipande cha nyama kitawawezesha kuishi kwa siku moja zaidi.
Nchi jirani ya Zimbabwe imefuata mkondo huo, na kuamua kuwaua tembo 200 ili kulisha watu walioathiriwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa.
Hatari ya uhifadhi mazingira
Kama inavyotarajiwa, mpango wa kukabiliana na ukame wa Namibia umeibua hisia kali kutoka kwa wahifadhi, ambao wanauona kama suluhu la muono mfupi na lisilo lenye tija.
Mwanataaluma Julian (sio jina lake halisi) anasema kuwa zoezi la kuchinja wanyamapori lisingeweza kupunguza uhaba wa chakula.
"Ni dhahiri kwamba nyama itasambazwa haraka, na matumizi yake pia yatakuwa ya haraka," anaiambia TRT Afrika.
"Tatizo ni: Unafanya nini baadaye?" Kundi la kutetea haki za wanyama la PETA limetuma barua kwa Waziri Mkuu Saara Kuugongelwa-Amadhila, ikieleza kinachofanya hatua hiyo kuwa "si ya kikatili tu bali pia ya hatari isiyokuwa ya kikmkakati".
"Haitakuwa na athari za muda mrefu kwa matatizo haya magumu," makamu wa rais wa PETA Jason Baker anasema katika barua hiyo, iliyowekwa kwenye tovuti ya shirika.
PETA ina wasiwasi kuwa udukuzi huo unaweza kusababisha kukosekana kwa usawa katika mifumo ya ikolojia, hali ambayo imesababisha baadhi ya wahifadhi kutishia kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Mauaji hata ya tembo wachache yanaweza kuharibu mifugo yote, na kusababisha vifo vingi miongoni mwa walionusurika na migogoro ya mara kwa mara na hatari ya binadamu na wanyama," Baker anaonya katika barua hiyo iliyotumwa kwa Waziri Mkuu.
Kundi la wahifadhi wa Kiafrika, pia, wametoa taarifa ya pamoja wakielezea wasiwasi wao juu ya mauaji ya wanyama wengi nchini Namibia, wakisema inaweka historia ya kuwezesha serikali "kunyonya wanyamapori wanaolindwa na mbuga za kitaifa chini ya kivuli cha mahitaji ya kibinadamu".
Taarifa hiyo inahoji ikiwa tathmini yoyote ya athari za mazingira ilifanywa kabla.
Mzozano msituni
Serikali imesajili huduma za wawindaji wa kitaalamu kwa ajili ya uchinjaji. Uidhinishaji wa awali kutoka kwa wizara ya mazingira ni uchinjaji wa viboko 30, nyati 60, swala 50, tembo 83, nyumbu 100, swala 100 na pundamilia 300.
Wengi wa wanyama hao wanatoka katika mbuga za kitaifa zinazolindwa nchini.
"Kuhusu kukosolewa kwa uingiliaji kati wa serikali ya Namibia, tunataka tu kusema kwamba mashirika ya NGOs hizi za Magharibi pengine hazielewi ukali wa hali nchini," anasema Muyunda.
"Mwisho wa siku, Namibia ni nchi huru. Tunafanya maamuzi kulingana na kile tunachohisi ni bora kwa watu wetu, na wale wanaokosoa - kimsingi, wengi wao - tayari wameangamiza wanyamapori wao."
Lakini Julian anahofia hili ni suluhisho ambalo litaleta matatizo zaidi kwa jamii ya Namibia.
"Hatua hiyo inaweza kupunguza njaa ya watu kwa muda lakini ikazua hali ya utegemezi. Watu watatarajia serikali kuendelea kusambaza chakula hata baada ya ukame kuondoka," anasema.
Kwa hiyo, ni njia gani iliyo bora zaidi kutokana na hali halisi ya ukame wenye kudhoofisha?
Julian anaitaka serikali kuanza kufikiria hatua za kukabiliana na hali hiyo kwa muda mrefu na kuwapa watu ujuzi wa kujitegemea ili taifa liweze kujilisha kabla, wakati na baada ya ukame kama huu.
Namibia ilitangaza hali ya hatari mwezi Mei kutokana na ukame ambao tangu wakati huo umekumba mataifa mengi Kusini mwa Afrika.
Hali ya ukame, kati ya msururu wa athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo dunia italazimika kukabiliana nayo zaidi, imesababisha uzalishaji wa nafaka kushuka kwa asilimia 53 na kiwango cha maji ya bwawa kushuka kwa asilimia 70 ikilinganishwa na mwaka jana.
Ni ukame mbaya zaidi Kusini mwa Afrika katika miongo kadhaa, kutokana na mchanganyiko wa hali ya asili ya El Nino - ongezeko la joto lisilo la kawaida la maji katika Mashariki ya Pasifiki - na joto ya hali ya juu linalosababishwa na uzalishaji wa gesi chafuzi.
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afŕika inakadiria kuwa watu wapatao milioni 68, au asilimia 17 ya wakazi wa kanda hiyo, wanahitaji misaada.
Umoja wa kikanda umeomba msaada wa dola bilioni 5.5 za Marekani kusaidia kukabiliana na ukame.