uwekezaji mkubwa umefanyika katika sekta ya uzalishaji ambayo imeongoza kwa miradi 377 yenye thamani ya kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 3.1/ Picha : X- TIC 

Kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania (TIC) kimesema kimesajili miradi 842 yenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni 7.7 mwaka 2024, hivyo kufikisha asilimia 88.2 ya malengo yake ya kusajili miradi 1000.

Mkurugenzi Mkuu wa TIC Gilead Teri alipowasilisha ripoti ya uwekezaji kwa mwaka 2024 katika mkutano na waandishi wa habari, amesema kuwa takwimu hizo, zinaonyesha kiwango kikubwa cha uwekezaji kuwahi kutokea tangu mwaka 1991.

Kwa mujibu wa Bw. Teri, ripoti hiyo inaonyesha uwekezaji mkubwa umefanyika katika sekta ya uzalishaji ambayo imeongoza kwa miradi 377 yenye thamani ya kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 3.1, ikifuatiwa na sekta ya usafiri iliyoingiza kiasi cha Dola bilioni 1.2, na kusajili miradi 138.

Sekta nyengine ambazo zinaonekana kufanya vizuri ni pamoja na sekta ya majengo ya biashara, yenye thamani ya Dola milioni 706, utalii iliyosajili miradi 76 yenye thamani ya Dola milioni 337, na ukulima ambao umesajili miradi 66 yenye thamani ya Dola milioni 599.

Uwekezaji huo, unatarajiwa kutengeza ajira mpya 248,078. Huku miradi 290 ikimilikiwa na wazawa.

TRT Afrika