Na Kudra Maliro
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Judith Suminwa, ameorodheshwa kuwa mwanamke mwenye ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika mwaka 2024 na Jarida la Forbes katika orodha yake ya kila mwaka ya wanawake wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani.
Forbes ilisema orodha hiyo iliamuliwa na vigezo vinne vikuu - pesa, vyombo vya habari, athari na nyanja za ushawishi.
Suminwa, 57, aliteuliwa na Rais Felix Tshisekedi mwezi Aprili 2024 kama waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa DRC baada ya kuchaguliwa tena.
Aliorodheshwa katika nafasi ya 77 ya mwanamke mwenye ushawishi mkubwa zaidi duniani katika orodha ya Forbes.
"Kutajwa kuwa mwanamke wa 77 mwenye ushawishi zaidi duniani na Forbes kunakwenda zaidi ya kutambuliwa kibinafsi. Ni ishara ya matumaini kwa kila msichana mdogo na mwanamke nchini DRC," alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X.
"Tuendelee kufanya kazi kuelekea siku zijazo ambapo kila mwanamke, nchini DRC na kwingineko, anaweza kutambua uwezo wake kikamilifu," aliongeza.
Hapo awali Waziri Mkuu alifanya kazi katika Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kama mratibu wa nguzo ya 'Kujenga Amani na Kuimarisha Demokrasia'.
Kazi yake ilikuwa mashariki mwa Kongo, eneo linalokabiliwa na ghasia zinazoendelea na ukosefu wa utulivu.
Mpumi Madisa
Mfanyabiashara wa Afrika Kusini Mpumi Madisa, 45, aliorodheshwa kuwa mwanamke wa pili mwenye ushawishi mkubwa zaidi barani na wa 87 duniani.
Madisa anaongoza Bidvest, kampuni ya huduma na usambazaji ya Afrika Kusini yenye wafanyakazi karibu 130,000 na soko lenye thamani ya dola bilioni 5.3.
Anachukuliwa kuwa shujaa baada ya kuwa mtendaji mkuu pekee wa kike Mweusi wa kampuni ya 40 bora katika Soko la Hisa la Johannesburg alipoteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa Bidvest mnamo 2020.
Anakaa kwenye bodi za kampuni 16 za kampuni tanzu, Forbes ilisema.
Ngozi Okonjo-Iweala
Mwanauchumi wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala, 70, aliorodheshwa mwanamke wa tatu wa Afrika mwenye ushawishi mkubwa zaidi mwaka 2024.
Mnamo Novemba, aliteuliwa tena kwa muhula wa pili kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Ulimwenguni.
Alikua mwanamke wa kwanza na Mwafrika wa kwanza kuhudumu katika nafasi hiyo mnamo Machi 2021.
Hapo awali, alihudumu kwa mihula miwili kama waziri wa fedha wa Nigeria, kuanzia 2003-2006 na 2011 hadi 2015.
Pia alihudumu kwa muda mfupi kama waziri wa mambo ya nje mwaka 2006.
Samia Suluhu Hassan
Rais wa kwanza mwanamke Tanzania Samia Suluhu Hassan, 64, aliorodheshwa kuwa mwanamke wa nne mwenye ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika na 91 duniani, kwa mujibu wa orodha ya Forbes.
Aliteuliwa kuwa rais kutoka nafasi ya makamu wa rais Machi 2021 kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.
Mnamo Septemba 2021, alikua kiongozi wa tano tu wa kike wa Kiafrika kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Forbes ilisema.
Mmiliki wa vyombo vya habari wa Nigeria Mo Abudu, 60, ni mwanamke wa tano kwa ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika na wa 97 duniani. Forbes ilimtaja kama mmoja wa wanawake wenye nguvu zaidi katika vyombo vya habari vya kimataifa.
Mnamo 2006, Abudu alianzisha Ebonylife TV, mtandao ambao sasa unaonyeshwa katika zaidi ya nchi 49 barani Afrika, na vile vile nchini Uingereza na Karibiani.
Mkataba wa kampuni yake na Netflix ulikua mara ya kwanza kwa kampuni ya vyombo vya habari barani Afrika kutia saini makubaliano ya filamu na TV yenye mada nyingi na kampuni hiyo kubwa.