Watawala wa kijeshi wa Niger wametangaza kufunga anga ya nchi hio na kuonya dhidi ya jaribio lolote la kukiuka hali hiyo kwani litakutana na "jibu la nguvu na la haraka".
"Kwa kukabiliwa na tishio la kuingilia kati, ambalo linazidi kuwa wazi kupitia maandalizi ya nchi jirani, anga ya Niger imefungwa kutoka siku hii ya Jumapili ... kwa ndege zote hadi ilani nyingine," walisema katika taarifa.
Maelfu ya wafuasi wa mapinduzi Niger walikusanyika kuwashangilia majenerali waliodai mamlaka, maktaa iliyowekwa na ECOWAS kwa jeshi kuachia madaraka au kukabiliana na uwezekano wa kuingiliwa kwa silaha umepita.
Muungano wa ECOWAS, unoasimamiwa na jirani ya Niger, Nigeria wenye nguvu za kijeshi za kikanda, ulikuwa umewapa wanajeshi waliomwondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum Julai 26 muda wa wiki kumrejesha madarakani.
Lakini Jumapili alasiri katika mji mkuu Niamey, maelfu ya wafuasi wa Baraza la Kitaifa linalotawala sasa la Ulinzi wa Nchi (CNSP) walijumuika kwenye uwanja uliokuwa umepambwa kwa bendera za Urusi na kubeba picha za viongozi wa CNSP.
Katika uwanja wa Seyni Kountche wenye viti 30,000, uliopewa jina la kiongozi wa kwanza wa mapinduzi ya Niger mwaka 1974, viongozi wa CNSP akiwemo Jenerali Mohamed Toumba walisalimiana na umati wa watu waliokuwa na furaha, huku wakionyesha kutokuwa na nia ya kuachia madaraka.
Wakuu wa jeshi la ECOWAS walikubaliana Ijumaa juu ya mpango wa uwezekano wa uingiliaji ili kukabiliana na mzozo huo, mojawpao ya mapinduzi ya hivi karibuni zaidi katika eneo la Sahel barani Afrika tangu 2020.
"Tunataka diplomasia ifanye kazi, na tunataka ujumbe huu upelekwe kwa uwazi kwao (wanajeshi) kwamba tunawapa kila fursa kubadili walichofanya," kamishna wa ECOWAS Abdel-Fatau Musah alisema.
Lakini alionya kwamba "vipengele vyote ambavyo vitaingia katika uingiliaji kati wowote vimefanyiwa kazi", ikiwa ni pamoja na jinsi na lini nguvu itatumika.
Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara alikariri wito kwa viongozi wa mapinduzi kujiuzulu Jumapili jioni katika mkesha wa Siku ya Uhuru wa nchi yake.
"Tunalaani jaribio la mapinduzi nchini Niger, ambalo ni tishio kubwa kwa amani na usalama katika ukanda huo," Ouattara alisema, huku akiongeza "ni muhimu" kwa "utaratibu wa kikatiba" kwamba Bazoum aliyechaguliwa kidemokrasia aruhusiwe kutawala.
Viongozi wa kijeshi wa Niger wamesema watajibu nguvu kwa nguvu.
Hisia kali dhidi ya Ufaransa
Eneo hilo linashuhudia ongezeka la hisia za kupinga Ufaransa, huku shughuli za Urusi, mara nyingi kupitia kikundi cha mamluki cha Wagner, zikiongezeka. Moscow imeonya dhidi ya kuingiliwa kwa silaha kutoka nje ya Niger.
Niger, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, inategemea sana misaada ya kigeni ambayo inaweza kuondolewa ikiwa Bazoum hatarejeshwa kama mkuu wa nchi, Paris imeonya.
Bazoum, 63, amekuwa akishikiliwa na viongozi hao wa mapinduzi pamoja na familia yake katika makazi yake rasmi ya Niamey tangu Julai 26.
Alishinda uchaguzi mwaka 2021 na kuanzisha uhamisho wa kwanza kabisa wa mamlaka ya Niger kutoka serikali moja ya kiraia hadi nyingine.
Nigeria tayari imekata usambazaji wa umeme kwa jirani yake Niger, na hivyo kuzua hofu kwa hali ya kibinadamu, wakati Niamey imefunga mipaka ya nchi hiyo kubwa ya Sahel, na kusababisha ugumu wa utoaji wa chakula.
Wanasiasa wakuu wa Nigeria wamemtaka Rais Bola Tinubu kufikiria upya uingiliaji kati wa kijeshi unaotishiwa.