Vita nchini Sudan vilianza Aprili 15 na vimewalazimisha watu kukimbia makwao   / Picha: AFP

Usitishaji vita wa saa 72 uliotiwa saini na pande zinazopigana nchini Sudan uliingia siku yake ya pili Jumatatu huku utulivu wa kiasi ukiripotiwa huko Khartoum na Darfur, maeneo ambayo yameathiriwa vibaya na mzozo huo.

Serikali za Saudi Arabia na Marekani, ambazo zilianzisha makubaliano hayo, zilisema siku ya Jumamosi kwamba usitishaji huo wa mapigano utaanza saa kumi na mbili asubuhi siku ya Jumapili.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia imesema usitishaji huo wa mapigano utatuliza mvutano na kuruhusu harakati na utoaji wa misaada ya kibinadamu.

Uchunguzi wa moja kwa moja siku ya Jumatatu ulionyesha kuwa sehemu nyingi za Sudan zilikuwa na utulivu, huku mlipuko na milio ya risasi kutosikika.

Vita nchini Sudan vilianza Aprili 15, wakati nchi hiyo ilipokuwa ikijiandaa kurejea kwa demokrasia ya kiraia baada ya zaidi ya miaka miwili ya utawala wa kijeshi.

Pande katika vita hivyo ni Jeshi la Sudan (SAF), linaloongozwa na rais wa mpito Jenerali Abdul Fattah al-Burhan, na Jeshi la Msaada wa Haraka, RSF, linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

Hadi sasa, zaidi ya watu 800, wakiwemo watoto 330, wameuawa, na wengine wasiopungua milioni 2.2 wameyakimbia makazi yao, huku nusu ya wakimbizi wakiwa ni watoto wadogo, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Ubalozi kushambuliwa

Kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya saa 72 kutiwa saini huko Jeddah, Saudi Arabia, makazi ya Balozi wa Tunisia mjini Khartoum, Shafik Hacci, yalivamiwa na kuporwa, wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia ilisema Jumapili.

"Shambulio hili ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kidiplomasia na kinyume na haki za kidiplomasia za makao makuu ya balozi za kidiplomasia," wizara ya Mambo ya Nje ilisema, ikidai shambulio hilo lilitekelezwa na vikundi vilivyojihami.

Tunisia ilitoa wito "kwa kuwashtaki wahusika wa kitendo hiki na kuwafikisha mahakamani".

Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika lilisema zaidi "mapigano yanapaswa kukoma mara moja na kwamba maslahi ya watu ndugu wa Sudan yanapaswa kuzingatiwa".

TRT Afrika