Zimbabwe imepokea kundi la kwanza la helikopta za Urusi ambazo zimekusudiwa kwa mashirika ya usalama na huduma za matibabu ya dharura.
Helikopta 18 zilizowasilishwa siku ya Alhamisi ni sehemu ya kundi la helikopta 32 zinazotarajiwa kutoka Rostec - shirika la serikali ya Urusi - kabla ya mwisho wa mwaka ujao.
Zitatumika "kwa ambulensi za anga, polisi wa anga na misheni ya uokoaji inapotokea majanga", kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali.
Rais Emmerson Mnangagwa alihudhuria sherehe siku ya Alhamisi ambapo helikopta hizo zilitolewa katika uwanja mkuu wa ndege katika mji mkuu, Harare.
Zimbabwe imekuwa mshirika wa karibu wa Urusi kwa miongo kadhaa na Rais Mnangagwa alisema uhusiano kati ya nchi hizo mbili "hauwezi kuvunjika, thabiti na umestahimili mtihani wa wakati".
"Nilipozungumza na Rais (Vladimir) Putin, alipendekeza kampuni yao itoe aina ya vifaa tunavyotaka na tumeagiza hivi 18," Bw Mnangagwa alinukuliwa akisema.
Hii inakuja miezi minne baada ya Rais wa Belarus Alexander Lukashenko, mshirika mwingine wa karibu wa Urusi, kutembelea Zimbabwe katika safari ambayo wizara ya mambo ya nje ilisema ililenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.