Marais wa nchi tofauti kutoka barani Afrika wameanza mkutano wa siku mbili, Saint Petersburg, Urusi katika mkutano wa pili wa Urusi na Afrika.
Rais wa Urusi Vladimir Putin aliuambia mkutano huo kwamba Urusi inaweza kuipa Afrika nafaka ambayo wamekuwa wakitoa Ukraine.
Alisema kuwa Moscow itakuwa tayari kuanza kusambaza nafaka bure kwa nchi sita za Afrika baada ya kati ya miezi mitatu hadi minne.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Burkina Faso, Zimbabwe, Mali, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Eritrea na kusema watapata tani kati ya tani 25,000 na 50,000 kila moja.
Urusi imesema pia iko tayari kufanya kazi na nchi za Kiafrika katika jitihada zao za kuanza kutumia sarafu za kikanda kwa ajili ya malipo, Rais Putin aliongeza.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, anatumai kuimarisha uhusiano na mataifa ya Afrika huku bara hilo likikabiliana na matokeo ya kujiondoa kwa Urusi katika mkataba wa mauzo ya nafaka wa Ukraine.
Urusi ilijiondoa katika mkataba wa mauzo ya nafaka wa Ukraine katika bara hilo, huku Putin akitarajiwa kutoa hakikisho kali.
Mkutano huo ni wa pili wa aina yake baada ya ule wa uzinduzi uliofanyika 2019 huko Sochi, kusini mwa Urusi.
Putin tayari amefanya maongezi ya moja kwa moja na marais kadhaa ambao wamehudhuria mkutano huo.
Mpango wa nafaka
Kwa muda wa mwaka mmoja, mpango huo uliruhusu takriban tani milioni 33 za nafaka kuondoka kwenye bandari za Ukraine, na kusaidia kuleta utulivu wa bei ya chakula duniani na kuepusha uhaba.
Moscow imetaka kuwahakikishia viongozi wa Afrika, ikisema inaelewa "wasiwasi" wao juu ya suala hilo na iko tayari kusafirisha nafaka bila malipo kwa nchi za Kiafrika zinazohitaji.
Kremlin inasema kuwa rais Putin anatarajiwa kuelezea maono yake ya uhusiano kati ya Urusi na Afrika na "kuundwa kwa utaratibu mpya wa dunia".
Putin pia atalijadili swala la vita Ukraine wakati wa chakula cha mchana na kundi la wakuu wa nchi za Afrika siku ya Ijumaa, Kremlin imesema.
Uwepo wa kundi la Wagner barani Afrika
Kuwepo kwa kikundi cha wanamgambo wa Urusi Wagner Group barani Afrika kunazua maswali na wasiwasi miongoni mwa mashirika ya kimataifa, Serikali za Afrika na mataifa ya kigeni
Wagner inatuhumiwa kuendesha operesheni haramu, kukiuka haki za binadamu na kuvuruga utulivu wa nchi za Afrika.
Kundi la Wagner limekuwa likifanya kazi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu 2018, kufuatia kusainiwa kwa makubaliano kati ya nchi hiyo na Serikali ya Urusi. Lakini Urusi, mara nyingi, imekataa uhusiano wowote na kikundi hiki.