Mwaka jana, Urusi iliuza nje takrian tani milioni 60 za nafaka, kulingana na rais Putin / Picha: Reuters

Waziri wa kilimo wa Urusi alisema kuwa Moscow imeanza usafirishaji wa bure wa nafaka unaofikia tani 200,000 kwa nchi sita za Afrika, kama alivyoahidi rais Vladimir Putin mwezi Julai.

Meli zinazoelekea Burkina Faso na Somalia tayari zimeondoka kwenye bandari za Urusi, na shehena za ziada kwenda Eritrea, Zimbabwe, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati zitafuata hivi karibuni, Dmitry Patrushev alisema katika taarifa iliyotumwa kwenye Telegram siku ya Ijumaa.

Putin awali ameahidi kupeleka nafaka za bure kwa nchi hizo sita katika mkutano wa kilele na viongozi wa Afrika mwezi Julai, mara tu baada ya Moscow kujiondoa katika makubaliano ambayo yaliiruhusu Ukraine kusafirisha nafaka kutoka bandari zake za Bahari Nyeusi licha ya vita na Urusi.

Mpango huo, unaojulikana kama mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi uliosimamiwa na Uturuki, ulikuwa umesaidia kupunguza bei katika soko la kimataifa.

Mwaka jana, Urusi iliuza nje karibu tani milioni 60 za nafaka, kulingana na Putin.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitaja ahadi za nafaka za bure "michango michache."

Nafaka kuharibiwa

Tangu kuacha mpango huo, Urusi imeshambulia mara kwa mara bandari za Ukraine na hifadhi za nafaka, na Kyiv inasema mamia ya maelfu ya tani za nafaka zimeharibiwa, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Hata hivyo, Ukraine ilisema Ijumaa kuwa imeweza kusafirisha tani milioni 4.4 za shehena zikiwemo tani milioni 3.2 za nafaka kupitia ukanda mpya wa meli iliyoanzisha mwezi Agosti.

TRT Afrika