Waandamanaji wa Nigeria walipeperusha bendera ya Urusi wakati wa maandamano ya hivi karibuni ya mageuzi ya utawala. / Picha: mtandao wa X

Urusi imejiweka mbali na habari za waandamanaji wa Nigeria wanaopeperusha bendera ya Urusi wakati wa maandamano yanayodai mageuzi ya utawala katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakiandamana hapa na pale, wakitaka kuona hatua kutoka serikalini ambazo zitapunguza gharama ya maisha na kudhibiti mfumuko wa bei.

Maandamano hayo yalianza rasmi tarehe 1 Agosti na yamesambaa kote nchini, huku idadi ya vifo, majeraha, na visa vya uharibifu wa mali vikiripotiwa katika baadhi ya majimbo.

Watu wasiopungua saba wamethibitishwa kufariki katika maandamano hayo na mamia kukamatwa tangu maandamano hayo yalipoanza mwishoni mwa wiki iliyopita.

'Hatuhusiki'

Idadi ya vifo inaweza kuwa juu zaidi kwani vyombo vya habari tofauti nchini Nigeria vinatoa takwimu tofauti, huku asasi ya kimataifa, Amnesty International, ikieleza kuwa idadi ya vifo ni 13.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Ubalozi wa Urusi nchini Nigeria ulisema umetoa taarifa katika vyombo vya habari vya Nigeria na kusambazwa kwa video na picha mtandaoni zikionyesha waandamanaji katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo wakiwa na bendera za Urusi na kuimba kauli mbiu za Rais wa Urusi Vladimir Putin.

"Serikali ya Shirikisho la Urusi pamoja na maafisa wowote wa Urusi hawahusiki na shughuli hizi na hawaziratibu kwa njia yoyote," ubalozi huo ulisema.

"Kama kawaida, tunasisitiza kwamba Urusi haiingilii mambo ya ndani ya mataifa ya kigeni, ikiwa ni pamoja na Nigeria. Haya ni maamuzi binafsi ya baadhi ya waandamanaji kupeperusha bendera za Urusi, na hayawakilishi msimamo rasmi au sera ya Serikali ya Urusi katika suala hili."

'Dhihirisho la demokrasia'

Urusi iliongeza kuwa inaheshimu "demokrasia ya Nigeria na inaamini kwamba maandamano ya amani yanayozingatia sheria za Nigeria ni dhihirisho la demokrasia. Hata hivyo, ikiwa matukio haya yatasababisha vurugu au vitendo vya ghasia, tunavikemea vikali."

Hivi karibuni, Urusi imepata kukubalika zaidi barani Afrika baada ya mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi, ikiwa ni pamoja na Mali, Burkina Faso na Niger, kuibua hisia za kupinga Ufaransa.

Niger na Chad pia zimewafukuza wanajeshi wa Marekani kutoka katika ardhi zao.

Wakati maandamano ya Nigeria yakiendelea kwa wiki nyingine, Rais Bola Tinubu alisema katika hotuba kupitia njia ya televisheni Jumapili kwamba amewasikia waandamanaji "kwa sauti kubwa na wazi."

Amri ya Kutotoka Nje

Hata hivyo, hakueleza kama atabadilisha sera zake za kiuchumi.

Wakati Rais Tinubu alipoingia madarakani Mei 2023, aliondoa mpango wa muda mrefu wa ruzuku ya mafuta, ambao ulikuwepo ili kudumisha bei za mafuta na gharama za uzalishaji kuwa chini.

Majimbo kadhaa, ikiwa ni pamoja na Borno, Yobe na Kano yenye watu wengi, yameweka amri za kutotoka nje kwa saa 24 baada ya maandamano huko kuwa ya vurugu.

TRT Afrika