Urusi itaanza kupeleka nafaka zake kwa nchi za Afrika ndani ya mwezi mmoja hadi wiki sita, shirika la habari la Interfax lilimnukuu Waziri wa Kilimo Dmitry Patrushev akisema Ijumaa.
"Sasa tunakamilisha hati zote. Nadhani ndani ya mwezi - au mwezi na nusu - zitaanza," Interfax ilimnukuu Patrushev akisema.
Rais Vladimir Putin aliwaambia viongozi wa Afrika mwezi Julai kuwa angewazawadia makumi ya maelfu ya tani za nafaka licha ya vikwazo vya Magharibi, ambavyo alisema vilifanya iwe vigumu kwa Moscow kuuza nje nafaka na mbolea zake.
Mwezi Julai, Urusi iliamua kutelekeza makubaliano ya mwaka mmoja ambayo yaliiruhusu Ukraine, mojawapo ya wauzaji wakubwa duniani, kusafirisha nafaka kutoka bandari zake za Bahari Nyeusi.
Nchi nyingi zimeathirika kwa ukosefu wa chakula cha kutosha tangu vita kuanza kati ya Urusi na Ukrain.
Miongoni mwa sababu nyingine za Urusi kukataa kuendelea na makubaliano ya kusafirisha nafaka ya Ukrain ni kuwa nchi za Magharibi zimekosa kutekeleza wajibu upande wao wa mkataba huo, uliowezeshwa kwa usaidizi wa Uturuki.
"Tutakuwa tayari kutuma nafaka Burkina Faso, Zimbabwe, Mali, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Eritrea tani 25-50,000 za nafaka za bure kila moja katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne ijayo," Putin aliuambia mkutano wa kilele wa Russia na Afrika wakati huo.
Hata hivyo mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa msaada kamahuo kutoka kwa Urusi ni tone katika bahari.