Taswira tofauti ilijitokeza katika kikao cha baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo mazungumzo juu ya Somalia yalimiminika nchi hiyo sifa na pongezi kwa hatua ilizopiga za kuweka utawala thabiti.
Mmoja baada ya mwingine wazungumzaji walitaja orodha ya mafanikio ya nchi hiyo huku wakitoa wito wa kuendeleza msukumo uliopo kuisaidia nchi hiyo isiteleze katika juhudi zake.
Catriona Laing, Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Somalia UNSOM, alielezea kuwa ameona mwenyewe mambo yalivyobadilika katika nchi hiyo.
‘’Nimejionea mafanikio makubwa Somalia katika Utawala na uimarishaji Amani,’’ aliongeza.
Bi Laing alisema kuwa kuna mabadiliko makubwa katika marekebisho ya usanifu wa usalama wa taifa na kuwekwa mifumo ya kuwezesha uchaguzi kufanyika.
Hata hivyo alisema kuwa ni muhimu kwa nchi hiyo kuendelea kuungwa mkono katika kukabiliana na wapiganaji wa Al Shabaab, sio tu kwa ajili ya usalama wa taifa hilo bali upembe wa Afrika kwa jumla.
Kwa upande wake, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, aliangazia juhudi kubwa za serikali kufikia muafaka na nchi wanachama kuhusu masuala mbalimbali, kukinga eneo hilo dhidi ya al-Shabaab na kupambana na ufadhili wa kigaidi.
"Niseme wazi, Somalia ya 2023 sio Somalia ya 1992," Hata hivyo, alisisitiza kwamba, licha ya maendeleo, safari ya nchi yake kuelekea amani na ustawi inakabiliwa na changamoto kubwa ya vikwazo vya muda mrefu vya silaha, vilivyowekwa nchini Somalia tangu 1992.
"Mkituondolea vikwazo hivi mutatuwezesha kuimarisha utawala wetu, kupambana na ugaidi ipasavyo na kujenga mustakabali wa amani na ustawi wa taifa letu".
Kauli yake inatilia mkazo wito kama huo kutoka kwa Umoja wa Afrika, waliolitaka baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuiondolea nchi hiyo vikwazo ili iweze kuimarisha ulinzi wake.
Ni mwaka mmoja tangu Hassan Sheikh Mohamud kushika usukani wa nchi na huku taifa hilo likiadhimisha miaka 63 tangu uhuru wake, wameendelea kupongezwa kwa ustadi wa maendeleo uliojitokeza.