Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM umelaani vikali shambulio la makombora lililomuua afisa wa Kitengo cha Ulinzi cha Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi.
"Kitengo cha Ulinzi cha Umoja wa Mataifa kina jukumu muhimu katika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi katika kuunga mkono amani ya Somalia na ujenzi wa serikali," alisema mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Catriona Laing.
"Tunalaani kitendo hiki cha unyanyasaji, na mawazo yetu yako pamoja na familia na wafanyakazi wenzetu walioathirika wakati huu mgumu,” Laing aliongezea,
Mashambulizi kadhaa ya makombora yalitua siku ya Alhamisi ndani ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde, ambapo Uwanja wa UN unapatikana.
Mbali na kifo cha mwanachama wa Kitengo cha Walinzi wa Umoja wa Mataifa, mashambulizi hayo yaliharibu miundombinu.
Al-Shabaab imeripotiwa kuhusika na shambulio hilo.
Umoja wa Mataifa nchini Somalia unatoa wito kwa wale waliohusika kufikishwa mahakamani, na bado wamejitolea kusaidia watu na serikali ya Somalia katika juhudi zao za kujenga amani na utulivu nchini humo.