Umoja wa Mataifa umeonesha wasiwasi juu ya ongezeko la uhasama wa kikabila na na vurugu zinazotokana na uchaguzi mkuu uliofanyika Disemba, 20 mwaka jana.
Ucheleweshwaji mkubwa wa kutangaza matokeo na urasimu ulitawala uchaguzi huo wa urais, wabunge, magavana na viongozi wa manispaa.
Hadi sasa, Tume ya Uchaguzi- CENI katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki imetangaza ushindi mkubwa kwa Felix Tshisekedi huku upinzani ukiuita uchaguzi huo kuwa ni kituko.
"Nimeshtushwa sana na hali ya kuongezeka kwa uhasama na uchochezi wa vurugu nchini Congo," amesema Volker Turk, Kamishna wa Haki za Binadamu ndani ya Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo, taarifa za uwepo wa vurugu baada ya uchaguzi, hasa katika maeneo ya Kivu ya Kaskazini na Kusini ni za kushtua mno.
Tshisekedi ni mzaliwa wa Kasai wakati hasimu wake mkubwa kisiasa anatokea Katanga, mji unaojulikana kwa uzalishaji mkubwa wa madini.
"Maneno ya chuki, ya kudhalilisha utu na ya uchochezi ni ya kuchukiza kwani yataongeza mvutano na vurugu katika DRC yenyewe, pamoja na kuweka usalama wa kikanda hatarini," alisema Turk.
Aidha, amezitaka mamlaka nchini Congo kuchunguza kwa uwazi taarifa na madai yoyote yanahusiana na maneno ya chuki na uchochezi wa vurugu na hata ikibidi kuwachukulia hatua wahusika.