Kikundi cha M23 kimedhibiti mji wa Goma  / Picha: Reuters

Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito wa kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Goma kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Inadai kuwa kuna umuhimu wa kufikisha misaada kwa watu katika eneo hilo haraka iwezekanavyo.

Mapigano makali kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kundi la wapiganaji la March 23 Movement (M23) yamesababisha athari mbaya kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma

Uwanja huo wa ndege ambao sasa uko chini ya udhibiti wa M23, ni ushahidi kamili wa kuwepo mapigano: ndege iliyoharibiwa ya Su-25 na injini yake ikiwa kwenye sehemu ya kuegesha ndege, helmeti nyingi zikiwa zimerundikana kwenye pembe moja ya uwanja wa ndege, magari ya kijeshi yaliyochomwa moto na ndege iliyokwama kwenye njia ya kupaa, pamoja na bunduki, mavazi ya kujikinga na risasi na makombora ya roketi yaliyoenea katika uwanja wote wa ndege.

Uwanja huo wa ndege ambao kwa sasa uko chini ya udhibiti wa M23, na kuna ishara kamili ya mapigano / picha: Wengine 

Mnamo Januari 27, M23 walidai kudhibiti Goma, mji mkuu wa Mkoa wa Kivu Kaskazini na eneo muhimu linalounganisha usafiri Mashariki mwa DRC, ikiwa hii ni hali mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 10.

Kwa sasa, mamia ya wanajeshi wa DRC bado wanazuiliwa katika kambi ya kijeshi karibu na uwanja wa ndege wa Goma.

Vikosi vya M23 vimekamata idadi kubwa ya magari na silaha nzito nzito katika uwanja huo wa ndege, huku baadhi ya silaha zikiwa tayari zinatumika na kundi hilo linalodai kuelekea kusini.

M23 sasa inaripotiwa kusonga mbele kando kando ya Ziwa Kivu kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Mkoa wa Kivu Kusini, takriban kilomita 200 kutoka Goma.

TRT Afrika