Makamu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) anayoshughulikia Miundombinu, Siasa na Jamii, Andrea Aguer Ariik Malueth ameongoza jopo la wajumbe kutoka jumuiya hiyo kutembelea umuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS).
Ziara hiyo inalenga kusaka uzoefu kutoka nchi wanachama za ECOWAS, yenye makao makuu yake mjini Abuja, Nigeria katika azma ya kukuza utangamano wa nchi za EAC.
Akizungumza baada ya kupokewa na mwenyeji wake Dr Omar Alieu Touray, ambaye pia ni Rais wa tume ya ECOWAS, Malueth amesisitiza umuhimu kwa nchi wanachama wa EAC kuchota uzoefu kutoka kwa wenzao, katika kufanikisha lengo la kukuza biashara na utangamano.
“Tuna imani kuwa EAC na ECOWAS zinaweza kubadilishana uzoefu, na kwa pamoja tunameza kuimarisha utangamano wa bara zima la Afrika,” ameeleza Malueth.
Jopo hilo kutoka EAC pia lilipata fursa ya kufanya mazungumzo na watendaji kutoka ofisi ya Makamu wa Rais wa ECOWAS kuhusu utekelezwaji wa maboresho ya kitaasisi ndani ya tume ya ECOWAS, katika miaka 10 iliyopita.
Ujumbe kutoka Arusha pia ulizungumza na Makamishna wanaoshughulikia Siasa, Ulinzi, Usalama, Nishati, Uchumi na Kilimo ndani ya Jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi.
Kwa namna ya pekee, pande zote mbili zilikubaliana kuendelea kushirikiana katika siku zijazo.