Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Serikali ya Kenya imependekeza jina la Veronica Mueni Nduva kuchukua nafasi ya Caroline Mwende Mueke katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. (EAC).
Hatua hiyo inakuja siku mbili kabla ya Mueke kuapishwa kama Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, yenye nchi wanachama nane.
Ikumbukwe kuwa, jina la Mueke lilipendekezwa na Rais wa Kenya, William Ruto kama mbadala wa Peter Mutuku Mathuki, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Urusi.
Mueke alitarajiwa kumaliza kipinchi cha miaka miwili cha uongozi wa mtangulizi wake.
Hata hivyo, Aprili 15, 2024, Serikali ya Kenya ilipitisha jina la Veronica Mueni Mwende kama mbadala wa Mweke ndani ya EAC, wakati Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo likikutana leo kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria, Katibu Mkuu wa EAC, anapaswa kuhudumu kwa kipindi cha miaka 5. Hata hivyo, Mathuki alikuwa amehudumu kwa miaka 3, katika nafasi hiyo ya juu ndani ya EAC, kabla ya maamuzi ya Machi 8, yaliyofikiwa na Rais Ruto.
Kulingana na itifaki ya kuanzisha EAC, Rais wa nchi husika anaweza kupendekeza jina kwa nafasi ya Katibu Mkuu, kabla ya kuidhinishwa na Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.
Nafasi hiyo huwa ni ya mzunguko kwa kila nchi mwanachama, na mteule huhudumu kwa muda wa miaka mitano.
Katika barua yake ya tarehe 15 Aprili, iliyotumwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC Deng Alor Kuol, Waziri wa Kenya anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Peninah Malonza hakutoa sababu ya Rais Ruto kupendekeza jina la Mwende kuchukua nafasi ya Mweke.
Kwa sasa, Nduva ni Katibu Mkuu katika Idara ya Wizara ya Utumishi wa Umma nchini Kenya.
Wakati huo huo, serikali ya Uganda imeridhia uteuzi wa Nduva kama Katibu Mkuu mpya wa EAC.
Kupitia ukurasa wake wa X, Waziri wa Afrika Mashariki nchini Uganda, Rebecca Alitwala Kadaga amesema kuwa Baraza la Mawaziri la EAC limepitisha jina la Nduva katika nafasi hiyo.