Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliongoza marais wengine kukutana na rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: AP

Ujumbe wa viongozi wa Afrika unaolenga kufanya upatanishi kati ya Urusi na Ukraine umemwambia rais wa Urusi Vladimir Putin kuwa ni wakati wa kujadiliana na Ukraine kusitisha kwa mapigano.

Ujumbe huo uliokutana na Putin Jumamosi, ulihusisha marais kutoka Senegal, Afrika Kusini, Zambia na Comoros, pamoja na waziri mkuu wa Misri.

Walikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy Ijumaa.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Saint Petersburg, rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye anaongoza ujumbe huo, alisema,

''Tuko hapa kuwasilisha ujumbe wa wazi kabisa kwamba tungependa vita hivi vikomeshwe, mgogoro huu lazima utatatuliwe.''

Ramaphosa alitoa wito wa mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine kumaliza mzozo huo kwa sababu ya madhara yake ya kimataifa hasa kwa nchi za Afrika.

''Huu ni wakati wa pande zote mbili kujadiliana kumaliza vita,'' Ramaphosa aliongeza.

Kiongozi wa Afrika Kusini pia alihimiza ''kufunguliwa kwa usafirishaji wa nafaka katika Bahari Nyeusi'' hadi kwenye soko la kimataifa.

''Njia za nafaka na bidhaa lazima zifunguliwe sokoni. ''

Ujumbe wa Afrika ulitaka watoto wote walionaswa katika mzozo huo warudishwe walikotoka, lakini Putin alisema Urusi haizuii watoto wowote wa Ukraine kurejea nyumbani.

"Tuliwatoa katika eneo la migogoro, kuokoa maisha yao," Putin alisema.

Je, mazungumzo ya Urusi na Ukraine yanawezekana?

"Tumekuja kukusikiliza na kupitia kwako kusikia sauti ya watu wa Urusi," alisema Rais wa Comoros Azali Assoumani, ambaye kwa sasa anaongoza Umoja wa Afrika.

"Tulitaka kukuhimiza kuingia katika mazungumzo na Ukraine," alisema.

Kwa upande wake, rais Vladimir Putin alisema Urusi iko tayari kuzingatia mapendekezo yoyote ya Afrika kwa ajili ya kupata suluhu na Ukraine lakini alidai ni Kyiv inayokataa mazungumzo hayo.

''Tulikubali mara moja pendekezo lenu la kufanya mazungumzo kuhusu suala la Ukraine,'' rais Putin aliuambia ujumbe wa Afrika.

Putin alisema Urusi "iko tayari kwa mazungumzo yenye thamani na mtu yeyote ambaye anataka kuanzisha amani kwa misingi ya haki na kwa kutambua maslahi halali ya pande husika."

Hata hivyo, Urusi imesema mara kwa mara kwamba suluhu yolote lazima izingatie "uhalisia mpya", ikimaanisha Urusi imemiliki majimbo matano ya Ukraine, manne kati yake ambayo inayadhibiti kwa kiasi.

Viongozi wa Afrika wamependekeza kuwa baada ya ujumbe huu, wataendelea na juhudi za upatanishi huku wakitafuta makubaliano kati ya pande husika kwa "hatua za kujenga imani" .

Ukraine wiki iliyopita ilianza mashambulizi ya kulazimisha vikosi vya Urusi kutoka eneo la Ukraine walilovamia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alikuwa amesema baada ya kukutana na viongozi hao mjini Kyiv siku ya Ijumaa kwamba mazungumzo ya amani na Urusi yatawezekana kwa sharti kuwa Moscow iyaondoe majeshi yake katika ardhi ya Ukraine.

TRT Afrika