Mawakili wa serikali ya Uingereza wanatarajiwa Jumatatu kuwasilisha rufaa yao katika mahakama kuu wakiomba kutengua uamuzi wa awali kuwa ni kinyume cha sheria mpango wa kuwafukuza wahamiaji Rwanda, mojawapo ya sera kuu za Waziri Mkuu Rishi Sunak.
Mwezi Juni, Mahakama ya Rufaa ya London ilihitimisha kuwa mpango wa kupeleka makumi ya maelfu ya wahamiaji zaidi ya maili 4,000 (kilomita 6,400) hadi Afrika Mashariki haukuwa halali, ikisema Rwanda haiwezi kuchukuliwa kama nchi ya tatu salama.
Mahakama iliamua kwamba wale waliotumwa Rwanda watakuwa katika hatari ya kurudishwa nyumbani ambako wanaweza kukabiliwa na mateso licha ya kuwa na madai halali ya hifadhi.
Hilo litafanya sera hiyo kuwa kinyume cha sheria chini ya Sheria ya Haki za Kibinadamu ya Uingereza (HRA), ambayo ilifanya Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu (ECHR) kuwa sehemu ya sheria za Uingereza.
Sera hiyo ya serikali ya Uingereza imesababisha mtafaruku mkubwa ndani na nje ya nchi hiyo huku wengi wakilalamika kuwa ilifikiwa bila mashauriano muafaka na wahusika wote.
Pigo kwa serikali ya Conservative
Mbali na pendekezo la kuwafukuza wahamiaji, serikali ya Rishi Sunak pia ilileta hatua nyingine ya kuwafungia wanao tafuta hifadhi katika boti kubwa wasiingie ardhi
Uamuzi huo wa awali wa mahakama ulileta pigo kubwa kwa ahadi ya chama vha Conservative cha Waziri Mkuu Sunak ya kuwazuia maelfu ya wahamiaji kuwasili kwa boti ndogo kwenye pwani ya kusini ya Uingereza.
Kwa muda wa siku tatu wiki hii, serikali itapinga katika Mahakama ya Juu ya Uingereza kwamba uamuzi huo haukuwa sahihi, huku wale wanaowakilisha wahamiaji kutoka Syria, Iraq, Iran, Vietnam na Sudan wakitaka majaji kuhitimisha mpango huo wenyewe ni kinyume cha sheria.
Sera ya kuwapeleka wahamiaji Rwanda ilitangazwa kwa mara ya kwanza mwaka 2022.
Fidia kwa Rwanda
Kupitia sera hiyo Uingereza Ilipanga kuwa watu wanaofika nchini humo kwa “njia zisizo halali, hatari au zisizo za lazima,” kama vile kwa mashua ndogo zinazovuka mfereji wa English Channel, wapelekwe Rwanda ili kutafuta hifadhi yao huko.
Kwa upande wake Rwanda ilikuwa inapokea mamilioni ya dola kuweza kufadhili upokeaji na uhifadhi wa wakimbizi hao.
Hatua hii ilipingwa vikali na watetezi wa haki za binadamu, waliotilia shaka historia ya Rwanda kuhifadhi haki za binadamu.
Ndege ya kwanza ya serikali ya Rwanda iliyopangwa kuhamishwa ilikuwa inatakiwa kuondoka mwezi Juni mwaka jana, lakini ilizuiwa dakika za mwisho kwa amri ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu hadi hatua zote za kisheria za Uingereza kukamilika.