Ugonjwa usiojulikana umeikumba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC. Shirika la Afya Duniani, WHO, limetuma wataalamu wake nchini humo kusaidia kuchunguza ugonjwa huo mpya ambayo haueleweki.
Kati ya Oktoba 24 na Disemba 5, 2024, katika eneo la Panzi katika Jimbo la Kwango DRC jumla ya maambukizi 406 ya ugonjwa huo yaliripotiwa.
Wataalam wa afya wanasema walioambukizwa wana dalili kama homa, maumivu ya kichwa, kikohozi, mafua na maumivu ya mwili. Walioambukizwa pia wameripotiwa kuwa na utapiamlo mkali.
Zaidi ya vifo 79 vitokanavyo na ugonjwa huo vimesajiliwa. Maambukizi mingi yameripotiwa kwa watoto, hasa walio chini ya umri wa miaka mitano.
WHO inasema ufikiaji wa eneo lililoathiriwa ni mgumu hasa wakati wa msimu wa mvua kwa sababu ni mbali na mjini. Kulifikia eneo hilo kutoka mji mkuu wa DRC Kinshasa kwa njia ya barabara inaweza kuchukua takriban saa 48.
Changamoto hizi, pamoja na uchunguzi mdogo katika kanda, zimechelewesha kutambua sababu kuu za ugonjwa huo.
Timu za wataalamu kwa sasa zinakusanya sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara, kutoa maelezo ya kina zaidi ya kliniki ya maambukizi yanayogundulika, kuchunguza mienendo ya maambukizi, na kutafuta kikamilifu iwapo kutakuwa na maambukizi ya ziada, ndani ya vituo vya afya na katika ngazi ya jamii.
Hii sio mara ya kwanza kwa DRC kukumbwa na maambukizi ya magonjwa sugu. Tangu 1976 nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa rasilimali barani Afrika, imepambana na milipuko 14 ya Ebola.
Mwaka huu wa 2024, DRC imeathiriwa na mlipuko wa Mpox, ambao umeathiri zaidi ya watu 4900 na kuwauwa wengine zaidi ya 625.
Na sasa kuibuka kwa ugonjwa huu usiotambulika kunaletwa changamoto mpya kwa mamilioni wa raia wa nchi hiyo, ambao asilimia kubwa wanaishi katika umaskini.