Wizara ya Afya imesema virusi hivyo viligunduliwa kwa mtu mmoja aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda kwenda Rwanda kupitia Kenya / Picha: Reuters

Kenya imethibitisha kisa cha kwanza cha Mpox katika mpaka wa Taita Taveta na Tanzania.

Wizara ya Afya imesema virusi hivyo viligunduliwa kwa mtu mmoja aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda kwenda Rwanda kupitia Kenya.

Maambukizi, ambayo husababishwa na virusi vya monkeypox, huenea kwa kuwasiliana kwa karibu, na kusababisha dalili za mafua na upele wa maumivu. Kesi nyingi ni nyepesi lakini zinaweza kuua.

"Nawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji au kitakasa mikono. Ikiwa una dalili, pata ushauri wa afya na epuka kuwasiliana kwa karibu na watu wengine ... epuka kuwasiliana kwa karibu na watu wenye ugonjwa unaoshukiwa au uliothibitishwa," Wizara ya Afya ilisema katika taarifa.

"Maambukizi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwengine yanaweza kutokea kwa kugusana moja kwa moja na ngozi iliyoambukiza au vidonda vyengine kama vile mdomoni au kwenye sehemu za siri. Ugonjwa huo pia unaweza kuambukizwa kupitia matone ya kupumua."

Visa vya ugonjwa huo unaoambukiza kwa kasi vimegunduliwa hivi karibuni nchini Rwanda na Burundi, huku aina mpya ikienea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ilitoa tahadhari kwa nchi wananchama kuhusu ugonjwa huo baada ya Burundi kupatikana na visa vitatu vya Mpox.

Tangu Mei 2022, mlipuko wa Mpox kwa nchi nyingi umekuwa ukiendelea duniani kote huku visa vya juu zaidi mnamo Agosti 2022 na Juni-Novemba 2023.

TRT Afrika