Na Kevin Philips Momanyi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Mnaukumbuka wimbo wa ‘Stella Wangu’?
Humo ndimo Freshley Mwamburi, kutoka Kenya alimoweka hisia zake za dhati kwa binti mrembo aitwaye Stella, ambaye alimlipia ada wakati anasomea udaktari huko Japan.
Mwimbaji huyo kutoka kaunti ya Kilifi iliyoko eneo la pwani ya Kenya, anasimulia namna alivyouza kila alichokuwa nacho ili kugharamia masomo ya Stella, na kuishia kuambulia patupu kwa kumsaliti na kijana wa Kijapani.
Wimbo huo, uliorekodiwa na kutolewa mwaka 1992 na bendi ya Everest Kings, umekonga nyoyo za wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki, na si ajabu kusikia ukirudiwa mara kwa mara, kwenye kumbi za burudani.
Kila ifikapo Mei 17, ya mwaka Wakenya huukumbuka wimbo wa ‘Stella Wangu’, kwani ndio siku rasmi Stella aliyoahidi kurudi na kumshangaza Freshley.
“Ilikua tarehe kumi na saba mwezi wa tano ndiyo ilokua tarehe kamili ya Stella kurudi Kenya. Nilikwenda uwanja wa ndege kwenda kumlaki Stella. Nilikua na uncle Kilinda uwanja wa ndege. Nilikua na Baziri mwa Kolomba na mkewe na watoto wake….. Ghafla ndege ilipotua uwanjani tuliona vituko," ni sehemu ya kibwagizo cha wimbo huo
Freshley anawahimiza wenzake kupitia wimbo huo, kwenda kumpokea Stella kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, kabla ya kushikwa na butwaa baada ya kipenzi chake kushuka kwenye ndege akiwa na mwanaume kutoka Japan na mtoto mwenye asili ya Kijapani.
"Stella alishuka amebeba mtoto mkononi nyuma yake mchumba wake mfupi Futii nne Mjapani Nilisikitika ndani ya moyo Nikakosa la kufanya Nilitamani nilie Kikamba lakini sikijui," anaendelea Freshley.
Akiwa mwenye huzuni kubwa, Freshley alielekea studio akiwa na mwanamuziki mwenzake Abdul Muyonga wa Everest Kings, wakarekodi wimbo maarufu wa Stella, ambao ulibeba jina la albamu ya Stella!