Ufilipino imeripoti maambukizi yake ya kwanza ya Mpox mwaka huu, lakini idara ya afya bado haijaamua iwapo ni ile aina mpya ya hatari inayozua taharuki duniani.
Ugonjwa hatari na unaoambukiza zaidi unaojulikana kama 'Clade 1b' umeua mamia ya watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kupatikana nchini Uswidi na Pakistan katika siku za hivi karibuni.
Shirika la Afya Ulimwenguni wiki iliyopita lilitangaza kuongezeka kwa mpox kuwa dharura ya afya ya umma ya wasiwasi wa kimataifa, kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari.
Mwanamume huyo Mfilipino mwenye umri wa miaka 33 ambaye aliambukizwa virusi hivyo, hakuwa amesafiri nje ya nchi, hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Jumatatu ya idara ya afya. Kesi yake iliripotiwa katika hospitali ya serikali Jumapili.
Kulingana na mamlaka ya Afya Afrika, CDC, Mpox imeathiri takriban mataifa 12 ya Afrika yakiwemo mataifa ambayo hayajaathirika hapo awali kama Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda.
Kufikia sasa, nchi hizo zimethibitisha maambukizi 2,863 na vifo 517, haswa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Maambukizi yanayoshukiwa katika bara zima yamepita 17,000, ongezeko kubwa kutoka 7,146 mwaka 2022 na maambukizi 14,957 mwaka 2023.