Utafiti uliotolewa Oktoba 25 na jarida la New York Times unaonesha Harris na Trump wanalingana kwa asilimia 48./Picha: TRT World  

Na Brian Okoth

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Siku ya Novemba 5, taifa la Marekani litamchagua Rais wa 47 katika historia ya nchi hiyo.

Mtifuano huo utamkutanisha Makamu wa Rais Kamala Harris kutoka chama cha Demokrat dhidi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump, ambaye atakuwa anapeperusha bendera ya chama cha Republican.

Wagombea wengine katika uchaguzi huo ni pamoja na mwanaharakati wa kisiasa Chase Oliver kutoka chama cha Liberty, daktari Jill Stein kutoka chama cha Kijani na Cornel West ambaye anasimama kama mgombea huru.

Hata hivyo, macho na masikio yote yako kwa Harris na Trump.

Upigaji kura mapema

Watu wapatao milioni 244 wanategemewa kushiriki kupiga kura kwenye mchakato huo.

Nchini Marekani, zoezi la kupiga kura hufanyika kwa njia ya masanduku ya kura au kwa njia ya barua pepe.

Utafiti uliotolewa Oktoba 25 na jarida la New York Times unaonesha Harris na Trump wanalingana kwa asilimia 48.

Mbali na kumtafuta Rais, uchaguzi wa Novemba 5 pia utakuwa utasaka viti 435 katika bunge la nchi hiyo na vingine 34 kwa ajili ya bunge la seneti.

Sifa za wagombea wakuu

Harris, ambaye amehudumu kama makau wa rais wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka minne, aliwahi kuwa seneta na mwanasheria mkuu wa jimbo la California na mwendesha mashitaka wa San Francisco.

Mgombea huyo anasaka nafasi ya kuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo.

Rais wa zamani Trump anagombea kwa mara ya tatu, akiwa ameshinda kiti cha Urais mwaka 2026 kabla ya kukikosa mwaka 2020.

Trump ni Rais wa 45 wa Marekani akiwa pia amejijengea jina kwenye ulimwengu wa biashara na uigizaji.

Ahadi kwenye kampeni

Je, ni kipi ambacho kimeahidiwa na wagombea hawa?

Mipango ya kiuchumi ni pamoja na punguzo la kodi, udhibiti wa bei, unafuu wa makazi na kodi ya mtoto.

Kwa upande wake, Trump ameapa kupunguza kodi, kuanzisha kodi kwenye bidhaa ziingiazo nchini Marekani na kulinda mifuko ya kijamii. Trump pia ameweka ahadi ya "kulinda vibarua kwa ajili ya Wamarekani pekee"."

Ukosefu wa ajira nchini Marekani umefikia asilimia 4.1, huku watu milioni 7 wakiwa wameondolewa makazini.

Uhamiaji

Katika kampeni yake, Trump pia ameahidi "kuwarudisha wahamiaji nchini mwao."

Harris kwa upande wake, anaunga mkono wazo la kuajiri mawakala wa ulinzi mipakani na kufunga kabisa mpaka, ikiwa patatokea ongezeko la wahamiaji.

Rais Joe Biden alijitoa kwenye kinyang'anyiro cha Urais wa Marekani mnamo Julai 21 kufuatia shinikizo kutoka kwa wanasiasa wa Demokrat na wafuasia wake.

Akitoa sababu za kujiuzulu, rais huyo alisema kuwa alihofia kuwa kugombea kwake kungekuwa "kizuizi " kwa Wanademokrasia na kwamba kipaumbele chake kikuu kilikuwa "kumshinda" Trump katika uchaguzi wa Novemba.

Ni rahisi sana kumshinda Harris: Trump

Baada ya kujiondoa kwenye mbio hizo za Urais, Biden alimuidhinisha makamu wake Harris kama mpeperusha bendera ya Demokrat.

Na ilipofika mwezi Agosti, chama cha Demokrat kilimpitisha Harris kama mgombea ambaye atamvaa Trump kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba.

Trump alikaririwa akisema kuwa itakuwa ni rahisi sana kumshinda Harris tofauti na ingekuwa kwa Biden.

Mgawanyo wa wapiga kura Marekani

Kwa upande wa idadi ya watu, jumuiya ya Wazungu nchini Marekani ndiyo kubwa zaidi, kwa karibu asilimia 58; ikifuatiwa na Walatino kwa asilimia 19 na Waafrika wakiwa ni asilimia 12.

Hivyo basi, Rais wa Marakeni anachaguliwaje?

Marekani, ambayo mji mkuu wake ni Washington DC ina jumla ya majimbo 50.

Kila jimbo lina wawakilishi kwenye chombo maalumu ambacho kina sifa za kumpigia kura Rais.

Wapiga kura hawa huchaguliwaje?

Kwanza kabisa, kuna kura ya wananchi, ambayo inahusu kura ambayo wananchi walipiga moja kwa moja kwa wagombea urais.

Kwa mfano, ikiwa mgombeaji atashinda kura 'maarufu' katika Jimbo la California, atapiga kura zote za chombo hicho. California ina kura 54 za Chuo cha Uchaguzi.

Iwapo mwingine atashinda kura maarufu za Florida, atachukua kura zote 30 za Chuo cha Uchaguzi huko.

Namba ya maajabu 270

Majimbo ya Maine na Nebraska, hata hivyo, yanawapa wapiga kura kwa kutumia mfumo wa uwiano.

Kila jimbo kati ya 50 hupata wapiga kura wengi kwa kuzingatia idadi ya viti vyake vya Congress. Hii ina maana kuwa kuna baadhi ya majimbo yenye wapiga kura wengi kuliko mengine.

Washington DC, ambayo haina uwakilishi katika Congress, ina kura tatu za uchaguzi, na kufanya jumla ya wapiga kura kufikia 538.

Mshindi wa kinyang'anyiro cha urais anahitaji zaidi ya nusu ya 538 - yaani, walau kura 270 za chombo cha Uchaguzi - ili kushinda.

TRT Afrika