Rais wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ni moja katika ya viongozi wa Afrika waliompongeza Donald Trump./Picha: Wengine

Viongozi mbalimbali barani Afrika wamempongeza Rais mteule wa Marekani, Donald Trump kufuatia ushindi wake katika uchaguzi uliofanyika Novemba 5, 2024.

Donald Trump anatarajiwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani baada ya kuzoa zaidi ya kura 270 za baraza la wapiga kura.

Katika ukurasa wake wa X, Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud alisema kuwa anampongeza Rais mteule wa Marekani kwa ushindi wake wa kihistoria, huku akionesha shauku ya kuendeleza uhusiano baina ya nchi hizo mbili kwa nia ya kukuza amani, usalama na maendeleo.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi alituma salamu zake za pongezi kwa Donald Trump kwa ushindi wake mkubwa, akisisitiza nia ya DRC kuendelea kushirikiana na kiongozi huyo mpya wa Marekani katika kukuza uhusiano wa nchi hizo.

Rais Burundi, Evariste Ndayishimiye alimpongeza Trump, huku akiiuita ushindi huo kuwa kihistoria, pia akimtakia heri na fanaka katika uongozi wake.

"Nakutakia kila la heri unapoanza kuiongoza Marekani kwa mafanikio. Natumai tutaendelea kukuza ushirikiano wa nchi zetu," alisema Rais Ndayishimiye.

Katika salamu zake, Rais William Ruto wa Kenya amempongeza Donald Trump baada ya kuchaguliwa kama Rais wa 47 wa taifa la Marekani.

Kwa upande wake, Hakainde Hichilema wa Zambia amempongeza Trump kufuatia kuchaguliwa kama Rais wa 47 wa Marekani.

"Salamu za heri kwa ndugu zetu wa Marekani kufuatia ushindi wa Donald Trump. Mafanikio haya ya kihistoria yanaonesha uhuru wa watu kuchagua viongozi wao. Tunategemea kuendelea kukuza uhusiano wa nchi zetu," aliandika Rais Hichilema kupitia ukurasa wake wa X.

Naye Rais wa Baraza la mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alimtakia kila la heri Rais huyo mpya wa Marekani, huku akiangazia ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika