Tume Huru ya Uchaguzi nchini DRC (CENI) imesema kwamba zoezi la kupiga kura litaendelea hadi Disemba 21 jioni, ili kutoa fursa kwa waliokosa kupiga kura siku ya Jumatano. Hii inatokana na baadhi ya vituo kuchelewa kufunguliwa hivyo upigaji kura kuchelewa kuanza kutokana na changamoto za vitendea kazi.
Hata hivyo, hatua hiyo, tayari imepata upinzani mkali kutoka kwa wagombea wa upinzani watano wakiwemo Martin Fayulu na Denis Mukwege ambao wanasema CENI haina mamlaka ya kikatiba au kisheria kuongeza muda wa kupiga kura.
Wapinzani wengine wanataka Uchaguzi uahirishwe na CENI itoe tarehe nyingine itakayokubaliwa na wagombea wa vyama vyote.
Vituo kadhaa havikupata mashine za kilektroniki kwa ajili ya kupiga kura kwa muda. Pia vipo vituo vilipata mashine lakini vilikosa nyaya maalumu za kuunganisha mashine hizo.
Vituo vilivyoanza kupiga kura mnamo majira ya saa 2:00 asubuhi hapo jana, hadi kufikia saa kumi na moja jioni bado wapiga kura wengi walikuwa wamesimama kwenye foleni kusubiri kupiga kura.
Mbali na sheria ya uchaguzi ya DRC kutaka zoezi la kupiga kura lidumu kwa saa 11 pekee, CENI imethibitisha kuongeza muda wa siku moja kutoa nafasi kwa walioshindwa kupiga kura hapo jana.
Katika uchaguzi huo, rais Felix Tshisekedi anasaka muhula wa pili dhidi ya upinzani uliogawanyika.
Wananchi wa DRC wamepiga kura kuchagua rais, wabunge wa kitaifa na kikanda pamoja na madiwani wa mitaa.
Mnamo Jumatano, mkuu wa tume huru ya uchaguzi Denis Kadima, alitangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba maeneo ambayo hayakuweza kupiga kura siku hiyo yatapiga kura Alhamisi.
Kadima pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba "si chini ya asilimia 70" ya wapiga kura waliweza kupiga kura, lakini alisisitiza kuwa hii ilikuwa makadirio.