Mahakama ya Tunisia imemhukumu Rached Ghannouchi, mmoja wa wapinzani wakuu wa Rais wa Tunisia Kais Saied, kifungo cha mwaka mmoja jela kwa makosa yanayohusiana na ugaidi, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti.
Ghannouchi, 81, spika wa zamani wa bunge, alikamatwa mwezi uliopita kwa tuhuma tofauti tofauti, sehemu ya kile shirika la kimataifa la Human Rights Watch (HRW) ilichokiita wiki iliyopita kuwa ni hatua ya "kukiondoa chama kikubwa zaidi cha kisiasa nchini humo".
Alikuwa amefikishwa mahakamani kwa mashtaka yanayohusiana na ugaidi mwishoni mwa Februari baada ya kushutumiwa kwa kuwaita maafisa wa polisi "wadhalimu".
Kesi hiyo ni mojawapo ya kesi zilizotozwa na mamlaka dhidi ya Ghannouchi, ambaye chama chake cha Ennahdha kilikuwa kikubwa zaidi bungeni kabla ya Saied kuvunja bunge mnamo Julai 2021.
Yeye ni miongoni mwa zaidi ya wapinzani 20 wa Saied wa kisiasa, wakiwemo mawaziri wa zamani na wafanyabiashara, waliokamatwa tangu Februari.
Wasiwasi wa kimataifa
Kuzuiliwa kwake mwezi uliopita, pamoja na wengine, kuliibua wasiwasi wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kutoka Umoja wa Ulaya, EU, ambao ulikumbuka umuhimu wa "kanuni ya msingi ya wingi wa kisiasa".
Marekani ilisema kukamatwa huko "kunawakilisha hali ya kutatanisha inayofanywa na serikali ya Tunisia dhidi ya wanaodhaniwa kuwa wapinzani".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock aliwaambia waandishi wa habari kwamba Berlin imelichukuwa swala la kukamatwa kwa Ghannouchi "kwa wasiwasi mkubwa" na akaonya kwamba "mafanikio ya kidemokrasia Tunisia tangu 2011 lazima yapotee".
Saied, 65, anadai waliozuiliwa walikuwa "magaidi" waliohusika katika "njama dhidi ya usalama wa serikali".
Wapinzani wametaja vitendo vyake kuwa "mapinduzi" na mabadiliko ya mafanikio ya kidemokrasia ambayo yaliibuka baada ya ghasia za Arab Spring katika eneo hilo zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Muungano mkuu wa upinzani, National Salvation Front (FSN), ambayo Ennahdha ni mwanachama, ulisema wakati huo kwamba alikuwa akishikiliwa kwa tuhuma za "kupanga njama dhidi ya usalama wa serikali".
Ennahdha ilikataa nia yoyote ya Ghannouchi ya kuitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikisema "inalaani vikali uamuzi usio wa haki ambao unalenga kuficha kushindwa kabisa kwa mamlaka kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii".