Na Lulu Sanga
Maandamano makubwa yamefanyika katika mitaa mbali mbali Afrika kusini. Huku polisi wa kutuliza ghasia wakitapakaa katika miji na majiji hasa maeneo ya mjini ili kudhibiti machafuko ya aina yoyote.
Lakini je unapaswa kufahamu nini kuhusu maandamano hayo na nini kinaendelea sasa?
Siku ya jumamosi Julius Malema kiongozi wa chama cha upinzania cha EFF, chama cha tatu kwa ukubwa Afrika Kusini alitanga maandamano nchi nzima ya Afrika Kusini na kuwataka wafuasi wa chama chake kujitokeza kwa wingi ili kushinikiza mabadiliko.
“Siku ya tarehe 20 tutainyamazisha hii nchi kuonyesha ulimwengu mzima kuwa tunajali hali ya kitaifa ya nchi yetu na hatuwezi kukunja mikono yetu” ni kauli ya Malema kupitia video ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii mwishoni mwa juma lililopita.
Chama hicho kiliwataka wafanyakazi wasio wa lazima kusalia nyumbani au wajiunge na maandamano.
Idadi kubwa ya watu ilijitokeza siku ya jumatatu kama ilivyo azimiwa na kiongozi huyo wa upinzani hali iliyozua tafrani baina ya polisi na waandamanaji hao ambao walidhamiria kufanya maandamano ya amani na kuripotiwa kuwa zaidi ya watu 80 walitiwa mbaroni na polisi.
Sehemu za biashara zilifungwa na baadhi ya wakazi wa Afrika Kusini walibaki wamesalia nyumbani kutokana na ukosefu wa usafiri huku wengine wakihofia vurugu.
Je waandamanaji wanataka nini?
Chama cha upinzani cha EFF na waandamanaji wameainisha mambo kadha wa kadha ambayo kwao ni kero na wanataka kuona mabadiliko Afrika Kusini.
Kukatika kwa umeme mara kwa mara ni moja ya changamoto kubwa ambayo imesababisha kuibuka kwa maandamano hayo. Huku ikiripotiwa kuwa baadhi hukosa umeme majumbani kwa zaidi ya saa 10.
Kero nyingine kwa upinzania na waaandamanaji ni kukithiri kwa rushwa, uhaba wa maji na ukosefu wa ajira.
Hata hivyo msisitizo wao ni kung’oka madarakani kwa Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa, wakiainisha kuwa ameshindwa kuendesha nchi. Ambapo waandamanaji walitembea katika mitaa wakiwa wamebeba mabango yanayomtaka rais huyo ajiuzulu.
Je serikali ya Afrika Kusini inasemaje?
Siku moja kabla ya kufanyika maandamano hayo Rais wa nchi hiyo Ramaphosa alionya kuwa maandamano hayo si ya kawaida bali yanalenga kuipindua serikali yake.
Siku ya Jumapili Bunge la Afrika Kusini lilitangaza kuwa jeshi la nchi hiyo litatoa vikundi vya askari 3500 kwa kushirikiana na polisi kwa muda wa mwezi mmoja mpaka April 17 ili kudhibiti na kupambana na uhalifu.
Akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya haki za binadamu nchini Afrika Kusini, Rais Cyril Ramaphosa amegusia kuhusu baadhi ya kero zilizo ainishwa na waandamanaji lakini pia raia wa Afrika Kusini kwa ujumla.
Na amesema jukumu lake kama rais ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za muhimu.
“Kazi ambayo inafanywa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya kiuchumi na kijamii ni sehemu muhimu ya juhudi za kuboresha utoaji wa huduma kwa Waafrika Kusini wote. Hii ni pamoja na uwekezaji katika barabara na madaraja ya vijijini, miradi ya maji, na kupanua mtandao wetu wa umeme,” amefafanua Ramaphosa
Hata hivyo amesisitiza kuwa anatambua katika baadhi ya maeneo kuna wizi wa pesa za serikali na huduma hazitolewi. Lakini ameweka wazi kuwa yoyote anayehusika na wizi atakamatwa.
Pamoja na malalamiko hayo Rais Ramaphosa anasema kuwa takribani kaya milioni mbili maskini hupokea maji ya bure bila malipo, umeme bila malipo, na uondoaji taka bure bila malipo.