Na Kudra Maliro
"Kiasi cha Dola milioni 200 kimetengwa ili kuhakikisha huduma ya kujifungua ni bure nchini DRC," alisema Roger Kamba, Waziri wa Afya nchini DRC.
Bwana Kamba anathibitisha kwamba huduma ya kujifungua itakuwa bure kuanzia Jumanne hii huko Kinshasa, mji mkuu wa DRC.
"Kuanzia kwa mimba hadi mtoto kufikisha mwezi mmoja, kila kitu kitakuwa bure kabisa na serikali itahakikisha utoaji wa huduma. Zaidi ya hospitali 300 tayari zimechaguliwa katika jiji la Kinshasa na vifurushi zaidi ya 2190 vya kujifungulia kwa vituo vya uzazi tayari vimeshapatikana," aliongeza Waziri wa Afya ya Umma.
Waziri wa Afya, Dk. Roger Kamba, alisema kuwa wanawake karibia 600,000 hujifungua kila mwaka huko Kinshasa, na milioni 4 kote nchini.
Kulingana na Wizara ya Afya ya Congo, ufadhili tayari upo, na bajeti ya kila mwaka ya Dola milioni 41.7 kwa Kinshasa, na rasilimali zinazohitajika zinatolewa kwa hospitali.
Namba (*151#) itawekwa ili kuongoza wanawake kuelekea hospitali karibu zaidi, na ufuatiliaji utahakikishwa na mamlaka za udhibiti na ukaguzi wa afya.
Mpango huu unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote na kupunguza vifo vya akina mama. Utapanuliwa hatua kwa hatua katika majimbo mengine, kufunika nchi nzima ifikapo Januari 2024.