Na Sylvia Chebet
Esther Njiru amesimama pembeni ya barabara ya changarawe, jua la asubuhi likimuangazia usoni.
Akiwa amebeba ndoo ya lita 20 kichwani mwake, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 65 anatembea taratibu akiwa anatoka kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia yake.
Usumbufu anaopitia Esther na jamii yake ya Tharaka Nithi inayopatikana katikati ya Kenya, unaelekea ukingoni kufuatia mpango wa kampuni binafsi ya kuchimba visima jirani na nyumba ya Esther, kama mfano wa miradi unaolenga kutoa huduma ya maji safi kwa jamii za vijijini za Kenya.
Maji yanayotolewa kwenye visima hivi, huingizwa kwenye matenki ya kuhifadhia maji na kuwekewa dawa ili kuondoa vijidudu. Baada ya hapo husambazwa kwenye mabomba yanayotumia nishati ya jua.
'Mabomba janja' hayo hutumia utaratibu wa malipo ya kabla kwa kutumia mfumo wa intaneti.
"Kwa sasa, jamii ya Tharaka Nithi inafurahia huduma za maji tofauti na ilivyokuwa hapo kabla. Mradi huu utabadilisha maisha yao, kwa tone moja baada ya lingine," Elisha Omega, mhandisi wa maji kutoka kampuni ya eWATER anaiambia TRT Afrika.
Malipo ya Kabla
Wananchi hao hutumia simu zao kwa kulipia maji, kabla ya kupata huduma hiyo .
"Tumezitembelea jamii hizi, tukiwafundisha namna mabomba haya yanavyofanya kazi," anasema Omega.
Esther ni kati ya watu wanaofurahia huduma hii ya aina yake". Ametoa kifaa chake kutoka kwenye nguo yake na kugusisha kwenye kichwa cha bomba kabla ya maji kutoka kwa kasi.
"Huu ni mfumo wa moja kwa moja. Hakuna maji yanayopotea kwani bomba hufunguka na kufunga kila baada ya matumizi," anaelezea Omega. "Unapata namba yako ya kipekee ya akaunti…Kwa kugusa tu kichwa cha bomba, maji yanaanza kutoka."
Kuenea kwa Huduma
Mradi huu endelevu unalenga kuwafikia watu zaidi ya watu milioni moja, ifikapo mwaka 2029.
Makazi ya Faith Makena, yako takribani mita 200 kutoka kwenye mradi huu. Anafuraha sana kwa sasa, kwani huduma hii iko karibu naye.
Faith alizoea kununua maji yasiyo salama kutoka kwa wachuuzi, hatua iliyomgharimu dola za Kimarekani 1 kwa takriban makontena manane ya lita 20. Kwa bei hiyo hiyo, sasa anapata maji ya kutosha kujaza vyombo 30 vya aina hiyo.
"Natumia maji kwa ajili ya kuoshea vyombo, kufulia nguo, kunywa, kupikia na kwa shughuli zingine za nyumbani," anaiambia TRT Afrika.
Uhakika wa Usafi
Waziri wa maji nchini Kenya, Zacharia Njeru amewakikishia wakazi wa maeneo hayo kuhusu usalama wa maji hayo, akisisitiza kuwa maji hayo yamewekwa dawa kwa njia za kisayansi.
Kwa upande wake, Gavana wa Tharaka Nithi, Muthomi Njuki anaamini kuwa mradi huwa utatatua changamoto zote za kiafya kwa wakazi wa maeneo hayo.
"Wakazi wengi wa Nkodi wamekuwa wakifurika katika zahanati ya Nkodi na maeneo mengine ya jirani hapa Tharaka Nithi, kwa sasa, suala hili litakuwa historia," anasema.
"Mtu yeyote asikushawishi kutonunua maji. Wanasema unaweza kuokoa shilingi mbili kwa kuchota maji ya mtoni, huo ni uongo kwani utakuwa umenunua ugonjwa."
Gharama zinazotozwa kwa huduma ya maji hayo hutumika katika ufundi wa vifaa vinavyotokana na miundombinu hiyo. "Lazima pesa fulani iwepo iwapo kutatokea hitilafu yoyote katika miundombinu hiyo," anasema Omega.
"Baadhi ya vifaa hutupa ishara ya kuharibika au kuvuja kwa pampu za maji. Timu ya mafundi hufika haraka kurekebisha hitilafu hizo."
Mzigo mkubwa wa Kijinsia
Kulingana na UNICEF, wanawake na wasichana duniani kote kwa pamoja wanatumia saa milioni 200 kutafuta maji kila siku, gharama ya fursa ambayo haizingatiwi sana.
Kwa wasichana, kuchota maji kwa ajili ya familia ni kazi ngumu, isiyolipwa ambayo inamaanisha muda mdogo unaotumiwa shuleni au kuacha shule kabisa.
Kwa wanawake, kutumia saa nyingi kwenye kazi hii ya kila siku kunamaanisha kutoweza kutenga muda kupata faida za kiuchumi. Hii, kwa upande wake, huongeza hatari yao ya umaskini.
Wakati Makena anaachana na jirani yake Esther, migongo yao imeinamia mbele, kwa uzito wa mizigo wanayobeba vichwani, ndivyo tumaini jipya la kuwapunguzia mizigo hiyo linavyochomoza.