Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Nchi za Afrika bado ziko mashakani katika utekelezaji wa dhana na 'Akili Mnemba,' umesema Umoja wa Mawasilino Barani Afrika (ATU).
Kulingana na umoja huo, nchi nyingi za Afrika zinapitia changamoto kubwa katika uhifadhi wa taarifa na matumizi ya teknolojia zilizopitwa na wakati.
Katibu Mkuu wa ATU, John Omo amesisitiza umuhimu wa serikali za Afrika pamoja na sekta binafsi barani humo kuwekeza hasa katika teknolojia ya 5G, akianisha utofauti wa uwekezaji huo kati ya nchi za Afrika na zile zilizoendelea kama Switzerland.
Kwa mujibu wa Omo, nchi ya Switzerland imewekeza kikamilifu katika teknolojia na miundombinu mingine, ikilinganishwa na nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
"Hiyo ndiyo safari ya bara la Afrika katika kuifikia dhana nzima ya 'Akili Mnemba,' amesema Katibu Mkuu huyo wa ATU, wakati wa mkutano wa World Mobile Congress, uliofanyika jijini Barcelona, nchini Hispania hivi karibuni.
Omo anasema kuwa bara la Afrika bado linasuasua katika kutekeleza dhana ya Akili Mnemba, kwani nchi nyingi bado zinawekeza katika teknolojia ya 3G na 4G, wakati nchi zilizoendelea zimepiga hatua na kufikia mitandao ya 5G.
Hata hivyo, ni nchi chache tu barani Afrika zilizoamua kutekeleza sheria za ulinzi wa taarifa kudhibiti uchakataji na matumizi ya taarifa binafsi, ikiwemo Tanzania na Kenya. Hata hivyo, bado inahitajika kutolewa elimu ya kutosha kwa umma, kuhusiana na fursa ambazo zinaletwa na teknolojia ya Akili Mnemba.
Pamoja na jitihada za utungaji wa sera na sheria, bado nchi nyingi katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara zina matumizi hafifu ya mtandao wa intaneti.
Taasisi ya GSMA inaripoti kuwa ni asilimia 25 tu ya wakazi wa Afrika wenye kutumia simu janja, ambayo ni chini ya asilimia 51 kidunia.
Katika ripoti yake ya robo ya nne ya mwaka 2023 iliyotolewa Januari 2024, Mamlaka ya Mawasiliano na Udhibiti Tanzania (TCRA) inasema kuwa ni asilimia 32.13 tu za simu hizo za kisasa ziko katika matumizi nchini humo.
Hali ya sasa ya miundombinu inapunguza ukubwa wa utayari wa nchi nyingi za Afrika kutekeleza dhana ya 'Akili Mnemba'
Tofauti na hali ilivyo katika nchi za Magharibi, Dausen anasema kuwa itachukua muda kwa nchi za Afrika kuanza utekelezaji wa 'Akili Mnemba,' kutokana na uwekezaji duni wa miundombinu na rasilimali katika eneo hilo.