Raia wawili wa Tanzania Clemence Felix Mtenga na Joshua Loitu Mollel ni miongoni mwa raia wa kigeni ambao mpaka sasa hawajulikana walipo tangu mgogoro wa Israel na Hamas kulipuka tarehe Oktoba, 7.
Clemence na Joshua, waliwasili Israel kama sehemu ya mpango wa mafunzo ya kilimo baada ya kuhitimu masomo yao ya Chuo Kikuu.
Wawili hao, waliwasili kutoka Tanzania wiki chache tu kabla ya vurugu kuzuka eneo la Gaza na walikuwa katika eneo la Kibbutz Nahal Ozko, lililopo mita 800 tu kutoka mpaka wa Gaza.
Ikithibitisha kukosekana kwa raia hao, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania imesema katika taarifa yake kwamba, wanafunzi hao walikuwa nchini Israel kwa ajili ya masomo.
"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazo taarifa za kupotea kwa Watanzania wawili nchini Israel ambao ni miongoni mwa vijana 260 waliopo nchini humo katika mafunzo ya kilimo cha kisasa."
"Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka mbalimbali nchini Israel inaendelea na juhudi za kuwapata vijana hao ili kuwaleta katika mazingira salama. Familia za vijana hao zimejulishwa kuhusu jitihada hizo na Serikali inaendelea kuwasiliana nao," Serikali ya Tanzania imesema.
Katika taarifa yake pia, Serikali ya Tanzania imesema imefanikiwa kuwarejesha nyumbani baadhi ya raia wake walioko Israel na tayari wamefika nyumbani.
"Watanzania 9 wanaoishi nchini Israel waliitikia wito wa mpango wa Serikali wa kuwarudisha nyumbani na tayari walipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tarehe 18 Oktoba 2023," ilifafanua taarifa hiyo.
Pindi tu mzozo huo ulipozuka, serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ilianzisha mpango wa raia wake kujindikisha katika ubalozi wa nchi hiyo uliopo Tel Aviv kwa minajili ya kuwaondoa kutoka nchini humo.