Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro./Picha: habarizote.co.tz

Serikali ya Tanzania imelipa kiasi cha dola milioni 4.2 (shilingi bilioni 11.3) kwa ajili ya kulipa thamani ya maendelezo yaliyofanywa na wananchi hao waishio karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Kiwango hiki kilikuwa ni kwa mujibu wa tathmini ya kitaalamu ya mali za wananchi iliyofanywa katika eneo hili, taarifa iliyotolewa Mei 15, 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi imesema.

Kulingana na Matinyi, mpaka, kufikia Aprili 30, 2024, jumla ya wananchi 1,666 kati ya 1,712 walikwishalipwa malipo yao yenye thamani ya shilingi bilioni 11.2 ambapo wananchi hao wameshaondoa uendelezaji waliokuwa wameufanya juu ya ardhi ya KIA na kuhama kwa hiari, ili kupisha shughuli za maendeleo za uwanja huo wa ndege wa kimataifa.

"Mpaka kufikia tarehe 14 Mei, 2024, ni wananchi 46 tu ndio waliokuwa hawajapokea malipo yao kwa sababu tofauti tofauti zikiwemo kukosa akaunti za benki; kutofautiana kwa majina yaliyo katika taarifa za malipo na yaliyopo benki; kukosekana kwa uthibitisho wa mirathi kwa wananchi wanaotakiwa kulipwa fidia," ameeleza.

Matinyi alisisitiza kuwa, lengo la serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwezi Juni 2024, kila mwananchi awe amechukua malipo yake. Ni vyema ikaeleweka wazi kwamba, wananchi ambao hawajachukua malipo bado wapo kwenye makazi yao ndani ya eneo la KIA.

Sehemu ya kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro./Picha: Africa Scenic Safaris

Kati ya mwaka 2007 na 2010 wananchi wa jamii ya wafugaji kutoka wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na Hai mkoani Kilimanjaro, walianza kuingia, kuweka makazi na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya eneo la KIA.

Shughuli hizo za kibinadamu zinazohusisha kilimo na ufugaji ndani ya eneo la uwanja zimekuwa zikiathiri shughuli za uendeshaji hasa katika kipindi cha kiangazi ambapo upepo wa vumbi na kusababisha uono hafifu kwa marubani kiasi cha ndege kushindwa kutua na hivyo kulazimika kwenda kutua kwa dharura katika viwanja jirani.

TRT Afrika