SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linalomilikiwa na Serikali, limelipa dola milioni 23.6 kuongeza mara mbili ya hisa zake katika kitalu cha gesi asilia cha Mnazi Bay chini ya makubaliano na kampuni ya nishati ya Ufaransa ya Maurel & Prom (MAUP.PA).
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, alisema katika hafla ya utiaji saini Jumamosi kuwa kampuni hiyo imeongeza umiliki wake wa kitalu hicho mara mbili hadi 40% baada ya kupata hisa za ziada za 20% kutoka kampuni ya Maurel & Prom.
Akishuhudia halfa ya kutia saini mauzo hayo, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, alipongeza kama hatua kubwa ya kulinda hifadhi za taifa kwa manufaa ya wananchi.
''Ununuzi wa hisa hizo utasaidia kuongeza mapato kwa TPDC na serikali, kuimarisha usalama wa nishati nchini kwa kuepuka sehemu kubwa ya kitalu kuendeshwa na kampuni moja,'' alisema Rais Samia.
Katika kuhakikisha hilo, Rais Samia aliagiza wizara ya nishati kuhakikisha sekta ya gesi asilia inakidhi mahitaji kwa bei nafuu ili itumike nyumbani, viwandani na kwenye vyombo vya usafiri.
''Mabadiliko ya tabianchi yamefanya mahitaji ya gesi na nishati nyingine mbadala kuwa kipaumbele katik akujenga uchumi shindani,'' alisema Rais Samia. ''Wizara haina budi kuongeza uzalishaji na usambazaji,'' aliendelea kusema Rais.
Awali kitalu hicho kilimilikiwa kwa pamoja na Maurel & Prom, TPDC na Wentworth Resources. Lakini baada ya Maurel na Prom kukubaliana kupata hisa za Wentworth Resources za asilimia 31.9, TPDC ilitumia haki yake kununua sehemu ya hisa iliyokuwa ya Wentworth.
Chini ya makubaliano hayo, TPDC na kampuni ya Maurel & Prom pia zilisaini mkataba wa pamoja wa uendeshaji ambapo TPDC itakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi katika uzalishaji na uendeshaji wa kitalu hicho, ikiwa ni pamoja na kupeleka maafisa wa serikali kuhudumu huko kwa muda mrefu.
Vile vile Rais Samia amesema kuwa serikali inaendelea kufanya jitihada maalum kuhakikisha raslimali za nchi ikiwemo gesi asilia zinawanufaisha wananchi wa taifa kikamilifu.
''Shabaha ya serikali ni kuendelea kunufaika zaidi na gesi asilia kwa kuhamasisha uzalishaji zaidi kwenye visima ambavyo tayari gesi imeshagundulika,'' alisema Mama Samia.
Kitalu cha gesi cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara, kusini mwa nchi hiyo, kina wastani wa futi za ujazo bilioni 641 za hifadhi ya gesi asilia inayoweza kurejeshwa na huchangia karibu nusu ya gesi inayotumika kuzalisha umeme katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.