"Watanzania tumetumia nguvu zetu na nguvu za awamu zote zilitumika mpaka hapa tulipofika." Asema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongeza, "Hii ni Ikulu ya Tanzania, mnakaribishwa wote."
Rais aliongea wakati wa uzinduzi wa Ikulu mpya Tanzania, iliyopo jijini Dodoma leo Jumamosi Mei 20, 2023.
Rais Suluhu alieleza kuwa safari hii haikuwa rahisi kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo changamoto za kiuchumi.
"Huu ni mradi wa pili wa John Pombe Magufuli niliyorithi, ya kwanza ikiwa Daraja la Tanzanite, na nitahakikisha nitaendeleza kazi aliyoanzisha na Mungu anipe uwezo wa kukamilisha yote. Tutaona pia michoro ya Samia complex."
Rais Samia aliwapongeza wote waliohusika na ujenzi wa Ikulu huku akisema "Kila mmoja katika eneo lake ametoa mchango mkubwa sana, na saa zingine mlifanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, hamkukata tamaa mliweka taifa mbele. Asanteni sana kwa kujitolea."
"Nitaendeleza mema yaliyopo, na kuboresha inapobidi... na kazi iendelee."
Rais wa awamu ya nne Mrisho Jakaya Kikwete pia alikuwepo akisema "Leo tumeweka historia!" na "kuhitimisha dhamira ya baba wa Taifa" ya kuhamisha makao makuu kutoka Dar es Salaam kuhamia Dodoma.
Rais Samia alimalizia kwa kusisitiza "Tutakapo maliza msalato na ujenzi wa nyumba zetu katika awamu wa pili wa ujenzi wa Dodoma hata wageni wa kimataifa tutawapokea hapa."
Mahali pa kujenga jengo jipya lilichaguliwa na Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere mapema miaka ya 1973.
Kazi za ujenzi zilianza miaka mitatu iliyopita wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais John Magufuli - ambaye alifariki Machi 2021 akiwa madarakani.
Ikulu mpya inazidi ile ya Dar es Salaam mara 15, ikiwa na zaidi ya ekari 8,473 na inakuja na hifadhi ya wanyamapori.
Leo Rais Samia Suluhu Hassan amepanda mti mmoja wa kumbukumbu ikiwa ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa Ikulu Chamwino kama ishara ya utunzaji wa mazingira na kuikijanisha Dodoma.
Dodoma inabadilika kwa kasi huku majengo mengi yakijengwa. Kutoka angani inaonekana kama tovuti moja kubwa ya ujenzi.
"Ikulu Mpya ya Chamwino ni kazi ya kodi za watanzania, jengo hili litunzwe vizuri na kusaidia Rais kufanya maamuzi mazuri kwa ajili ya watanzania." alisema Makamu wa Rais Philip Mpango wakati wa hotuba yake kwenye ufunguzi huo.