Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kali kwa viongozi wa taasisi na mashirika ya umma wanaozembea katika utenda kazi wao akisema kuwa kila mmoja atawajibika.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kwa wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma jijini Arusha, aliwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa taasisi zote zinajiendesha kwa tija na kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji kutoka serikalini.
''Ofisi ya msajili wa hazina ihakikishe taasisi zote zinaingia mikataba ya utendaji kazi na zinafanyiwa tathmini ipasavyo,'' aliongeza Rais Samia.
Rais pia alitangaza kufanywa mabadiliko makubwa katika uendeshwaji wa taasisi hizo, kuambatana na mapendekezo yaliyotolewa na afisi ya usajili wa hazina.
Miongoni mwa mabadiliko makubwa ni kufungwa kwa baadhi ya taasisi ambazo majukumu yake yanashabihiana au taasisi ambazo zimepitwa na wakati katika utenda kazi wao.
Hakikisho la ajira
Taasisi ambazo zinaonekana 'kulegalega' katika majukumu yake zitafanyiwa uchunguzi kuondoa changamoto zinazowakumba na wale walioonesha kujikimu na kuleta tija, watatuzwa.
Hata hivyo Rais Samia aliwahakikishia wafanyakazi hao wa umma kuwa kazi zao hazitafungwa.
''Wote ambao wako kwenye mashirika yatakayofungwa, aidha watamezwa kwengine au kutakuja mashirika mengine ambayo yana maana zaidi wakati huu,'' alisema Rais Samia. ''Kwa hivyo hakuna ajira itakayopotea. Naomba msihofu na msiogope mabadiliko.'' Aliongeza.
Takwimu zinaonesha kuwa 17% ya ajira ndani ya Tanzania inatolewa na mashirika au taasisi na wakala wa serikali.
Viongozi wa serikali wa ngazi za juu, wakiwemo mawaziri na makatibu wametakiwa pia kuyaacha mashirika yafanye majukumu yao kwa uhuru kwa mujibu wa sheria bila muingilio wa kisiasa.
Rais Samia waliwatahadharisha wanasiasa hao 'kutoingiza mikono yao' katika uendeshaji wa taasisi za umma ili bodi na wakurugenzi waweze kuwajibikia matokeo yao kamilifu.