Tanzania itaendelea kuheshimu mkataba wake na kampuni ya Adani, licha ya mmiliki wake Gautam Adani kukabiliwa na shutuma za utoaji hongo na udanganyifu, afisa mwandamizi wa Mamlaka ya Bandari amethibitisha.
Wiki iliyopita, Adani alishitakiwa kwa tuhuma za rushwa, huku hati za kukamatwa zikitolewa dhidi yake na mpwa wake.
Wawili hao walihusishwa na tuhuma za kula njama kuwahonga baadhi ya maofisa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 265, ili wapewe zabuni ya miradi ya umeme.
Hata hivyo, kampuni ya Adani imekana madai hayo.
Tanzania ilisaini mkataba wa miaka 30 na Adani Ports, kampuni tanzu ya Adani Group, kuendesha Gati ya Makontena 2 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mkataba huo pia ulijumuisha ununuzi wa asilimia 95 ya hisa za Kampuni ya Huduma za Gati za Makontena za Kimataifa ya Tanzania (TICTS) kwa dola milioni 95.
“Hatuna tatizo na mtu yeyote. Kila tunachopanga kukifanya kipo kwa mujibu wa sheria na makubaliano yetu,” alisema Plasduce Mbossa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika mahojiano yake na shirika la habari la reuters siku ya Novemba 26.
Kwa mujibu wa Mbossa, hakuna kasoro zozote kwenye mikataba waliyoingia na kampuni hiyo.