Mvua hizo mbali na kuharibu makazi lakini pia zimeharibu miundombinu ya barabara. Picha. TRT Afrika. 

Diana Wanyonyi

TRT Afrika, Tana River, Kenya

Mvua kubwa ya El-Nino inayoendelea katika mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki imesababisha maafa na madhara makubwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hizo.

Nchini Kenya, kaunti ya Tana River, Pwani ya nchi hiyo, imeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mafuriko huku ikiacha baadhi ya wananchi bila makazi.

Mito kadhaa ikiwemo Mto Tana umevunja kingo zake, hivyo kusababisha mafuriko katika vijiji kadhaa ikiwemo Tana Delta, pamoja na kuharibu miundombinu muhimu ikiwemo barabara na mifugo ya watu.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo, mpaka sasa watu 186,666 wameathirika na mafuriko, huku wengine 81,594 wameachwa bila makazi, watu 74,460 wakipata hifadhi kwa kambi mbalimbali. Tayari kuna kambi 84 zilizojaa wananchi waliokosa makazi katika kaunti hiyo ya Tana River.

TANA RIVER

Hapa njia ya usafiri ni kwa kutumia dau au boti ndogo.

Zilpa Moses ni moja wanawake aliyepata hifadhi katika kambi ya Kongolola, anasema japo alipokea chakula cha msaada, wanaomba msaada zaidi wa kibinadamu ili waweze kujimudu.

“Ingawaje mengine hatujapata lakini tunaomba sisi kina mama na watoto wetu angalau mtuangalie kwa misaada,” anasema Zilpa.

Bakari Bawati nae pia ni muathiriwa wa mafuriko katika kambi hii, anakiri kwamba wakazi wengi wanahangaika kimaisha.

“Hivi sasa tumeamka asubuhi tunashangaa, watu wameacha makao, hawana vyakula hawana chochote, wamebakia na kujazana mabarabarani. Watakula wapi? Kuna watoto wadogo hawana vyakula, sisi tunaomba msaada itufikie.” anasema Bawati.

Baadhi ya wakazi walio kambini wanasema hawana chakula. Picha/TRT Afrika. 

Boru Odicho ni mmoja wa wafugaji, anayekadiria hasara baada ya mifugo yake kufa kutokana na mafuriko.

“Mvua ni nyingi, kutakuwa na madhara sana, wakati wa ukame jua ikiwaka vizuri inabadilika, sasa mbuzi zimeanza kufa ni hasara,”nae anasema.

Gavana wa kaunti hiyo, Dhadho Godhana amesema wamepata suluhu ya kudumu ya kutatua mafuriko. Suluhu hiyo ni mpango wa kujenga vijiji vipya katika maeneo ambayo mafuriko hayafiki. Mradi huo mpya unaofahamika kama VILLAGE CLUSTER unalenga kujenga vijiji 48 vya kisasa.

“Tunatarajia kuwa asilimia 75 ya wanachi katika maeneo tofauti tofauti wataweza kufaidika na mpango huu. Wale watu ambao watakuwa katika vijiji vikubwa hawatahitajiwa kuhamia kwa clusters, yao itakuwa ni kuyaboresha maeneo, mipangilio ifanywe na wapewe ploti zao na waendelee kuishi. Tayari tushaanza hapa kugawanya ploti na tunatarajia kwamba kila tunapomaliza kuzigawa, wananchi watazidi kuhamia pale na kuendelea kuenga rasmi,” anafafanua Ghodhana.

Uongozi wa Kaunti ya Tana River unasema, umeanza kujenga vijiji vipya ili kuwahamisha wakazi wa maeneo yanayokabiliwa na mafuriko. Picha/TRT Afrika.  

Mwaka wa 2018 mafuriko yalisomba vijiji vingi eneo Tana Delta na kusababisha Serikali Kuu kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu kuwajengea wakaazi nyumba zilizogharimu shilingi billioni 1 ya Kenya, lakini zikabomolewa tena na mafuriko mwaka wa 2020.

Aidha, Mkurugenzi anayejishughulisha na masuala ya majanga katika Shirika la World Vision, Gershon Mwakazi anasema Shirika hilo tayari limetoa msaada kwa walioathirika na mafuriko.

“Kwa muda huu ambao imebidi watoke majumbani mwao, tumewapa vyandarua, vyombo vya kuchotea maji, mikeka na vyombo vya kupikia jikoni,” anasema Mwakazi.

Kati ya kambi 130 ambazo zimetengwa kama makao kwa waathirika wa mafuriko, kambi 95 ndizo zinatumika na waathiriwa hao.

Inakadiriwa kuwa takriban watu 175 wameaga dunia nchini Kenya kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua ya El-Nino. Mvua hiyo ilianza kunyesha kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.

TRT Afrika