Uhaba wa mashindano ya ndani umezorotesha ukuaji wa michezo ya kupigana./Picha: Wengine

Na Gaure Mdee na Charles Mgbolu

Mwamko wa sanaa za kujihami (MMA) unakua kwa kasi barani Afrika ambapo hadi sasa, nchi 19 zimeidhinishwa na MMA kuendesha na kusajili michezo hiyo.

Mchezo huu, ambao unatambulika kwa matumizi yake ya nguvu, huhitaji pia ujasiri, wakati ambapo majibizano ya ngumi na mateke hutawala.

Iwapo ni lazima utazame mchezo wa MMA, basi huna budi kujiandaa kisaikolojia, ukitazama ustahimilivu wa wachezaji hao wakitiririkwa na majasho.

Kwa sasa, baadhi ya nchi ambazo zimesajili na kurasimisha mchezo huu kwa ukanda wa Afrika, ni pamoja na Cameroon, Zambia, Algeria, Tunisia, Angola, Ghana, Morocco na Misri.

Hii inakuja wakati Afrika ina matumaini ya kupata waanzilishi wengine kwenye tasnia ya mchezo huu, kama Usman Kamaru, maarufu kama 'Jinamizi kutoka Nigeria', mwafrika wa kwanza kushinda tuzo za ya UFC, Machi 2019.

Ni katika kipindi hicho hicho, Mnigeria mwenzake Israel Adesanya, alishinda ubingwa wa uzani wa kati, pamoja na kwamba alikuwa anaiwakilisha nchi ya New Zealand.

Francis Ngannou, bondia wa zamani mwenye asili ya Cameroon aliyechukua uraia wa Ufaransa, pia anatajwa kama mwanamichezo mwenye ushawishi mkubwa kwenye tasnia ya MMA barani Afrika.

Mwaka 2021, Ngannou(37) alitwaa ubingwa wa uzito wa juu kwenye mashindano ya UFC.

Hata hivyo, safari ya kuipa uzito sanaa za kujihami imetawaliwa na changamoto za kutosha.

Kulingana na Chris Tibenda, nyota wa mchezo huo kutoka Tanzania, tasnia ya sanaa za kujihami inashindwa kukua kikamilifu kwa kukosa misingi imara.

Wanamichezo wengi wa MMA wanashindwa kupata mapambano ya kimataifa. Picha: Impact Wrestling 

"Tunao mabondia na wanamieleka wenye ujuzi na MMA, lakini kwa bahati mbaya, hawana jukwaa na ngazi stahiki zitakazokuza ujuzi wao na hatimaye kuwawezesha kushindana kimataifa, Tibenda anaiambia TRT Afrika.

Hali kadhalika, kuna upungufu wa michuano ya aina hii, na hivyo kudhoofisha jitihada za kutengeneza na kukuza vipaji.

‘’Wengi wa wanamichezo kutoka Nigeria kwa mfano, hawafikii hata mapambano saba kwa ujumla wao," anaeleza Henry George, Rais wa MMA nchini Nigeria, katika mahojiano na TRT Afrika.

Hata hivyo, kuna jitihada binafsi kutoka kwa wanamichezo wa MMA wenyewe kuhakikisha mchezo huu unavuka mipaka ya bara la Afrika.

‘’Watu wengi hawakufahamu uwepo wa sehemu za mazoezi kwa ajili ya MMA, Jujitsu na masumbwi, uelewa na mwamko ulianza kuongezeka mara tu baada ya watu kutambua kuwa hii ni zaidi ya michezo, bali ni mitindo ya maisha pia," anasema Tibenda.

Nchi ya Ghana kwa mfano, imeanzisha Chama Maalumu kinachoratibu michezo ya aina hii, kijulikanacho kama Wushu Martial Arts Association of Ghana.

Kwa upande wake, Afrika Mashariki imekuwa ikiandaa mashindano ya kanda, ikiwahusisha nyota wanaochipukia kama vile Tibenda mwenyewe na Rebecca Amongi kutoka Uganda.

Ngazi nyingine ya mashindano haya ni ile ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ijulikanayo kama Impact Championship, ambayo ni sehemu ya mashindano ya kando ya Afrika Mashariki ya MMA.

''Sisi ni kati ya nchi za kwanza kabisa barani Afrika kuidhinisha michezo ya aina hii, na leo tunashuhudia vijana wengi wakijihusisha na mchezo huu kuliko sehemu yoyote ile barani Afrika,’’ anasema Adam Mozer, promota wa MMA kutoka DRC.

‘’Tuna jumla ya vilabu 25 nchi nzima zenye vijana wapatao 1000, na zaidi ya yote, MMA inatambulika rasmi na serikali,’’ anaongeza.

Nchini Afrika ya Kusini, mchezo huu umewavuta washiriki wengi kutoka nje ya bara la Afrika, kama vile Scotland, Ufaransa na Ujerumani.

Mchezo huu pia, uliwakutanisha zaidi ya washiriki 20 kutoka kona mbalimbali barani Afrika, mjini Windhoek nchini Namibia mwaka 2022, kwa ajili ya tukio la kwanza, pekee la MMA.

Unyang'anyi wa damu

Tukio baya la unyang'anyi ndilo lililomfanya Chris Tibenda, kutoka Tanzania aingie kwenye mchezo huu.

Mchezo wa MMA unaendelea kung'arisha bara la Afrika./Picha: Impact Wrestling 

"Siku moja, nikiwa matembezini na dada yangu, nilivamiwa na kujeruhiwa vibaya na hao wanyang'anyi...toka siku hiyo niliamua kujifunza mchezo huu wa kujihami na imekuwa ndio sehemu ya maisha yangu," anaiambia TRT Afrika.

Hata hivyo, wataalamu wa MMA wanashauri kuwa msisitizo wa wa mchezo huu barani Afrika usiishie tu kwenye kushiriki kwenye anga za kimataifa tu, bali kukuza zaidi hadhi ya mchezo huu.

''Ndoto yangu ni kuona maendeleo mazuri ya mchezo huu. Na unapozungumzia maendeleo yake, ni vyema ukazingatia kuwa asilimia kati ya 80 na 90 ya wakufunzi wake wanatoka kwenye michezo mingine kama karate, judo na mieleka," anasema Henry George.

"Nataka kushinda mataji mengi zaidi ili niweze kuhamasisha watu wengi washiriki mchezo huu, kwani umenisaidia sio tu kuchanganika na watu wa kada tofauti, bali umeniwezesha kujilinda na kuwalinda wale niwapendao,'' anamalizia Tibenda.

TRT Afrika