Mamlaka ya afya ya Sweden imetangaza kisa cha ugonjwa wa Mpox.
Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya monkeypox.
" Mtu aliyetafuta katika eneo la Stockholm amegundulika kuwa na mpox iliyosababishwa na aina ya clade I. Ni kisa cha kwanza kilichosababishwa na clade I kukutwa nje ya bara la Afrika," mamlaka ya afya Sweden imesema.
Hii imekuja baada ya Shirika la Afya Duniani, WHO, kutangaza mpox kuwa Dharura ya Afya ya kimataifa huku kukiwa na visa zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi nyingine kadhaa za Afrika.
" Kama tulivyoona hapo awali, ilikuwa ni suala la muda tu kabla ya mpox aina ya clade I - ambayo inaonekana kuwa kali zaidi kuliko aina ya clade II - kugunduliwa katika maeneo mengine, tukizingatia ulimwengu wetu umeunganishwa," Hanks Kliuge , mkurugenzi wa WHO Ulaya amesema katika mtandao wao wa X.
Dalili za kawaida za mpox ni kutokea kwa vipele au vidonda vinavyoweza kudumu kwa wiki mbili hadi nne, ikiambatana na homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo, kupoteza nguvu mwilini na uvimbe mwilini.
Mamlaka ya afya ya Uswidi inasema mtu aliyeambukizwa alikuwa amesafiri kutoka eneo la Afrika ambalo kwa sasa limekumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
" Uswidi ina utayari wa kutambua, kuwatenga na kuwatibu watu wenye mpox kwa usalama," mamlaka hiyo imesema.
Kituo cha Afrika Udhibiti na Tiba ya Magonjwa barani Afrika (Afrika CDC) kinamsema kuwa kumekuwepo na visa 2,863 na vifo 517 katika nchi 13 kutokana na ugonjwa wa Mpox kwa mwaka 2024.