Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekataa pendekezo la jumuiya ya kikanda, Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD) kupeleka askari wa kulinda amani nchini humo ili kukomesha vita vilivyodumu kwa takriban miezi mitatu kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Kusaidia Haraka (RSF).
Katika taarifa yake siku ya Jumanne, wizara hiyo ililaani jaribio la ''kupeleka wanajeshi wowote wa kigeni nchini Sudan'' na kuonya kuwa itachukuliwa kuwa kitendo cha uchokozi dhidi ya nchi hiyo.
"Taarifa ya mwisho ya viongozi wanne wa (IGAD) katika mkutano wao mjini Addis Ababa ilijumuisha wito wa kufanyika mkutano wa Majeshi ya Dharura ya Afrika Mashariki (EAEF) kuzingatia uwezekano wa kupeleka vikosi kulinda raia na kuhakikisha mtiririko wa misaada ya kibinadamu,'' wizara ilisema.
"Katika suala hili, Serikali ya Sudan inathibitisha kwamba misaada ya kibinadamu inayotolewa na mashirika ya kimataifa inapita na kuwafikia wale wanaohitaji, na Serikali ya Sudan inabakia kuwa na nia ya kupunguza mateso ya watu wake na kuondokana na vikwazo vyote katika suala hili," wizara iliongeza.
"Serikali ya Sudan inathibitisha kukataa kupelekwa wanajeshi wa kigeni nchini Sudan na itawachukulia kama wavamizi," iliongeza.
Taarifa hiyo imelaani zaidi hotuba za Rais wa Kenya William Ruto na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwenye mkutano wa IGAD wa kutaka kutumwa kwa vikosi na kuziba pengo la usalama na uongozi nchini Sudan kutokana na vita vinavyoendelea.
Sababu ya uaminifu
Mapema wiki hii, viongozi wa kanda chini ya kambi ya IGAD walifanya mkutano ambapo walipendekeza kutumwa kwa vikosi vya kulinda amani nchini Sudan. Mkutano huo ulisusiwa na jeshi la Sudan huku wapinzani wake wa Rapid Support Forces wakituma mwakilishi.
Lakini wizara ya mambo ya nje ilisema jeshi la Sudan liko tayari kwa mazungumzo ya kutafuta suluhu la mzozo huo na kuongeza ''kilichoelezwa katika taarifa ya mwisho ya viongozi wanne kuhusu kutokuwepo kwa ujumbe wetu sio sahihi na si kweli.''
Jeshi la Sudan limekuwa namazoea ya kuwashutumu baadhi ya viongozi wa eneo hilo kwa kuhusika katika mzozo huo mbaya kati yake na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF.
''Kwa ajili ya uaminifu, ilitarajiwa kwamba taarifa ya vionmgozi hao inaonyesha kwamba kutoshiriki kwa ujumbe wa Serikali ya Sudan kunatokana na pingamizi lake la wazi dhidi ya uenyekiti wa Rais William Ruto wa kikao hicho ," wizara ya mambo ya nje ilisema.
Kulingana na wizara hiyo, "uwepo wa ujumbe wa Sudan mjini Addis Ababa kabla ya kuanza kwa mkutano na mawasiliano yake ya awali na mratibu wa mkutano huo ulithibitisha nia ya kweli ya Sudan ya kujihusisha katika kutafuta suluhu la mgogoro uliopo."