Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Sudan imeilaumu Serikali ya Kenya kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano wa kikundi cha Rapid Support Forces, RSF, kundi ambalo limekuwa likipigana na Jeshi la Sudan tangu Aprili 2023.
RSF iliandaa mkutano katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi Februari 18, 2025 uliohudhuriwa na ndugu wa kiongozi wa RSF.
"Kuwakaribisha viongozi wa wanamgambo wa kigaidi wa RSF na kuwaruhusu kufanya shughuli za kisiasa na uenezi wa propaganda, ni kuidhinisha mauaji ya kimbari, mauaji ya raia kwa misingi ya kikabila kushambulia kambi za waliolazimika kuhama makazi yao na kufanya vitendo vya ubakaji ni kuidhinisha uhalifu huu wa kutisha," imesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan katika taarifa yake.
Kundi hilo lilitangaza nia ya kutaka kuunda serikali mpya ya Sudan.
Hatua hiyo, imeikasirisha Serikali ya Sudan ambayo imesema inakiuka kanuni ya ujirani mwema lakini pia inakinzana na ahadi ambazo Kenya imetoa katika nyanja za kimataifa ya kutoruhusu shughuli za uhasama dhidi ya Sudan kufanyika katika ardhi yake.
Serikali ya Sudan imeonya kuchukua hatua zote muhimu dhidi ya maazimio yoyote yatakayofikiwa na RSF mjini Nairobi.
Lakini hii si mara ya kwanza kwa Kenya kujipata katikati ya makundi yanayozozana nchini Sudan.
Mnamo Juni 2023, Mamlaka ya Kitaifa ya Maendeleo IGAD, ambapo Sudan ni mwanachama ilichagua nchi 4 kuongoza jitihada za amani nchini Sudan.
Kenya na Sudan Kusini ziliongoza timu iliyojumuisha Ethiopia na Somalia.
Hata hivyo, kutokana na historia yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilikataa uteuzi wa Rais wa Kenya, William Ruto, kuwa mkuu wa kitengo cha nne kwa madai kwamba Kenya ina "upendeleo" kwa wanamgambo wa Kikosi cha RSF.
Mnamo Januari 2024 Rais William Ruto alikutana na kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo katika ikulu ya Nairobi, jambo ambalo halikuiridhisha serikali ya Sudan.
Mvutano huu huenda ukazua uhasama wa kidiplomasia kati ya Sudan na Kenya na hata kufanya upatikananji wa amani nchini Sudan kuwa mgumu zaidi kwani Kenya na Sudan ni wanachama wa IGAD na Umoja wa Afrika jumuia ambazo ziko mbioni kutafuta suluhu ya Sudan.